SHUGHULI ZA MUZIKI ENZI ZA MWALIMU NYERERE

Ni miaka 65 toka Tanganyika ipate Uhuru. Nchi sasa imepitia awamu 6 za uongozi wa juu wa serikali. Nimebahatika kuwa mwanamuziki katika awamu zote, leo ngoja niwasimulie ilikuwaje kuwa mwanamuziki enzi ya awamu ya kwanza, awamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mimi ni mzaliwa wa Iringa, nilipata bahati kuzaliwa katika nyumba ambayo muziki ulikuwa sehemu kubwa ya maisha. Moja ya starehe kubwa ya wazazi wangu ilikuwa muziki, baba yangu alikuwa na uwezo wa kupiga vyombo kadhaa vya muziki, vikiwemo, trumpet, saxophone, banjo, ukulele na gitaa kavu yaani lisilo tumia umeme. Yeye alirekodi kwa mara ya kwanza katika kituo cha redio pekee kilichokuweko wakati huo Tanganyika Broadcasting Services (TBC) mwaka 1960 na nyimbo hizo kupigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi kilichoitwa  Jimbo Letu, 16 May 1960, baba alilipwa shilingi 40 kwa nyimbo zake kurushwa redioni. Wakati huo ungeweza kununua gari jipya kwa shilingi 800, hivyo ni wazi kiwango kilicholipwa na redio hakikuwa kidogo. Huo ni ushahidi kuwa kabla ya Uhuru baadhi ya wanamuziki walikuwa wakilipwa mirabaha kazi zao zilipotumika katika redio.


Nikiwa na umri mdogo kabisa, nilianza kushirikishwa kuimba wakati baba akipiga gitaa na nilianza kuupenda muziki toka nikiwa na umri mdogo, na kwa kuwa nyumbani tulikuwa na radio na gramophone iliyokuwa na santuri za muziki aina mbalimbali,muziki wa Kiswahili, Kihindi, Kiingereza, muziki toka Afrika ya Kusini na muziki kutoka Kongo. Hivyo masikio yangu yalianza kusikia na kupenda muziki wa aina mbali.  Nilianza shule mwaka uleule ambapo Tanganyika ilipata Uhuru, nakumbuka siku moja kabla ya siku ya Uhuru, wanafunzi tulifagia barabara za jirani na shule yetu kisha kuzimwagia maji siku moja kabla ya Uhuru, ili siku ya Uhuru kusiwe na vumbi.

Shuleni kulikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Kuimba’, mwalimu alihakikisha anafundisha japo wimbo mmoja kwa wiki, vitabu maalumu vilikuwepo vikiwa na nyimbo zilizokuwa na mafunzo ya maisha, kuheshimu wazazi, wakubwa, kupenda shule na kadhalika. Somo hili lilikuweko katika ngazi zote za shule za msingi, na kulikuweko waalimu wengi waliokuwa wakijua hata kusoma na kuandika muziki kwa nota hivyo wanafunzi kupewa elimu ya muziki zaidi ya kuimba nyimbo.

Shule zote zilikuwa na ‘bendi’ ya shule.  Bendi ya shule, kila asubuhi bendi  ilipiga muziki wakati wanafunzi wakikaguliwa kama wamekuja shuleni wasafi, moja ya ndoto zangu  wakati huo ilikuwakuja kuwa mmoja wa wana bendi ya shule. Nilitamani aidha kuwa mpiga ngoma au mpiga filimbi na kubwa kuliko yote ni kupata bahati kuwa mshika kifimbo. Bendi hizi zilikuwa zikipiga muziki wa hali ya juu, waalimu waliokuwa na utaalamu wa muziki waliwezesha bendi hizi kuwa za kiwango cha juu cha upigaji. Shule zilishindana kwa kuzivalisha bendi mavazi bora na upigaji kuwa makini na hivyo siku za sikukuu kila shule ilijitahidi bendi yake ndio iwe bora. Hakika nakumbuka raha iliyokuwepo wakati shule mbalimbali zilipokutana siku ya siku kuu au kukiwa na maandamo na kisha kila bendi kupita mbele ya mgeni wa heshima, wanafunzi tulijitahidi kuwa wasafi, wakakamavu na wenye nidhamu ili shule yetu ishinde.  

Kila shule ilikuwa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili na nyingine kuwa na bendi za muziki wa kisasa. Nilisoma shule iliyokuwa na wahindi wengi, Iringa Aga Khan Primary School, bila kujali kabila wala utaifa wote tulicheza ngoma za asili. Hakika kulikuwa na Wahindi wanajua kucheza sindimba kuliko waswahili. Siasa ya Ujamaa iliingia wakati niko darasa la saba. Mambo mengi yalibadilika, nyimbo, ngoma ngonjera, mashahiri yalianza kuwa ni ya kisiasa, nyimbo nyingi za kiasili zikapewa maneno ya kisiasa, maafisa utamaduni ndio walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili, kwa kuzunguka kuhamasisha na hata kutoa adhabu kwa vikundi vilivyoonekana havitaki kuimba nyimbo za siasa. Bendi za kigeni ambazo zilikuwa zikitunga na kuimba nyimbo kwa lugha za kwao zililazimishwa kuanza kutunga na kuimba Kiswahili. Mashuleni tulianza kuimba nyimbo za siasa na za uzalendo kwa uwingi zaidi, somo la kuimba lilikuwa likifundisha nyimbo za siasa zaidi. Kwaya zilizokuwa na nyimbo mbalimbali za siasa na mafunzo mbalimbali kutoka kila upande wa nchi, zilirekodiwa na Radio ya Taifa ambayo kwa wakati huu ilikuwa imeshataifishwa na kuitwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Uzalendo ulikuwa ndio ‘habari ya mjini’.
Kila mwisho wa onyesho la muziki bendi zililazimika kupiga ule wimbo maarufu wa kukisifu chama ulioitwa ‘Chama chetu cha Mapinduzi cha jenga nchi’.
Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League) au TYL ulikuwa na matawi kila kona mpaka ngazi za vijiji na matawi haya ya TYL yalichangia sana kuendeleza muziki nchini, kwani kila kwenye tawi la TYL lazima kulikuwa na kundi la muziki aidha kwaya au ngoma, na mara nyingi vyote viwili. Kulikuwa na wilaya nyingi zilizokuwa na vyombo vya muziki wa dansi vilivyomilikiwa na  TANU Youth League, wanamuziki wengi maarufu wa miaka hiyo na ambao nyimbo zao bado maarufu mpaka leo walikotokea au walipitia bendi hizi za TYL.

Tangazo la gazetini

Pale Iringa, vyombo vya TYL hatimae viliishia kuwa chini ya shule ya Sekondari ya Mkwawa na shule hiyo ikawa na bendi nzuri sana ambayo iliweza kuja kurekodi RTD ikiwa na mtindo wao wa Ligija. Mashirika ya umma, taasisi mbalimbali za kiserikali zilihamasishwa kuwa na vikundi vya utamaduni ambavyo ndani yake kulikuwa na kwaya, bendi na ngoma za asili. Vingi vilikuja kuwa maarufu nchi nzima, kama vile vikundi vya Shirika la  BIMA la Taifa, vikundi vya majeshi yote Polisi, Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Wananchi , TANCUT, UDA, URAFIKI, NUTA na kadhalika. Pamoja na kutoa burudani vikundi hivi vilijenga uzalendo kwa vijana wa wakati ule.

Hasara moja kubwa ambayo lazima niiseme, ilikuwa ni kusisitiza kuwa vikundi hivyo vya muziki ni  kwa ajili ya kuelimisha na kuburudisha tu. Misingi ya biashara katika sanaa kwa ujumla haikutiliwa maanani. Pamoja na kuwa na wanamuziki wengi, hakukuwahi kuwa na kampuni binafsi ya muziki. Kampuni iliyokuweko iliitwa Tanzania Film Company. ILiweza kutoa santuri lakini usambazaji wake ulikuwa hafifu sana.  Nchi jirani ya Kenya na hata wakati fulani Zambia, zikabeba jukumu la kufanya biashara na muziki wa Tanzania. Bahati mbaya hata zama hizi, pamoja na viongozi kuendelea kusema muziki ni kazi na muziki ni biashara taratibu na sheria za uendeshaji wa shughuli hizi hazionyeshi nia hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top