Leo tunaendelea na safari ya kukumbuka bendi mbalimbali nchini, leo twende mkoa wa Mbeya. Tuanze na wilaya ya Mbeya, wilaya ambayo ni makao makuu ya mkoa siku hizi. Kabla ya mwaka 1927 wilaya hii ilikuwa ikijulikana kama wilaya ya Igali. Mji wa Mbeya ulianza  kupata umaarufu kutokana na kugundulika kwa dhahabu sehemu mbalimbali za kuzungukia mji huu kuanzia mwaka1906, hali iliyoendelea kwa karibu miaka ishirini baada ya hapo. Mji ukapata wageni kutoka kila kona ya Afrika Mashariki na Kati mpaka visiwa vya Ngazija, watu wakaja Mbeya na miji jirani kutafuta utajiri.
Popote penye vijana wengi, tena wakiwa wanatafuta pesa, hakukosekani burudani na hasa burudani ya muziki. Bahati mbaya si mengi yaliyohusu burudani za wakati huo yaliyowekwa kwenye kumbukumbu, lakini tuna taarifa nzuri tu za kiongozi na  mpenzi wa muziki aliyeitwa John Benedict Mugogo Mwakangale, mwenyewe alipendelea kuitwa JBM. JBM alikuwa pia mwanasiasa mashuhuri katika harakati za kupigania Uhuru na baadae katika siasa ya kutafuta umoja wa Afrika. Alifanya kazi kubwa ya kutambuliwa na hatimae alikuweko katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Tanganyika huru chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na akateuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Kazi, pia alikuwa Mbunge wa Nyanda za juu kusini,(siku hizi ni mikoa ya Iringa, Rukwa Njombe na Mbeya), kwa kipindi kirefu kabla ya Uhuru na hata baada ya Uhuru. Pamoja na yote hayo JBM pia alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki. Mwaka 1958 alikwenda Zambia, wakati huo ikiitwa Northern Rhodesia, alikwenda kununua vyombo vya muziki kwa ajili ya bendi yake iliyoitwa Free Mwakangale Jazz. Alipokuwa huko akakutana na vijana kutoka jimbo la Luanshya waliokuwa  na kundi lao la Three Brothers Band, walikuwa wakipiga vizuri sana muziki, Mwakangale akafurahishwa sana na kuongea nao li wajiunge na bendi yake. Hatimae wakakubaliana kuondoka kwao na kuingia Tanganyika kujiunga na Free Mwakangale Jazz, mmoja wa vijana hao aliitwa Michael Enoch.


Bendi ya Free Mwakangale Jazz makao yake makuu yalikuwa mji uliopewa jina la Neu Langenburg na Wajerumani lakini wote tunaufahamu siku hizi kama Tukuyu. Pamoja na Michael Enoch, Free Mwakangale Jazz ilikues na Ben Jack na Saiz Vera, hawa pia walitoka Zambia.  
Kuna hadithi ya kuchekesha na kusikitisha kuhusu kisa kilichofanya Free Mwakangale Jazz.
 Mwezi wa 9 mwaka 1958, Free Mwakangale Jazz ilipata safari ya kwenda Mwanza ambako kulikuwa na mkutano wa kwanza wa viongozi waliokuwa katika harakati za kutafuta uhuru kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, na katika mkutano huo kikazaliwa chama cha Pan-African Freedom Movement of East and Central Africa (PAFMECA). na baada ya kufika huko ilifanya maonyesho kadhaa, siku moja vijana hawa walikodi gari ili kubeba vyombo vyao, pengine wakati huo kwa ugeni na pengine hata Kiswahili walikuwa hawajakifahamu sawasawa, baada ya kujaza vyombo kwenye gari, dreva wa gari akawaomba wamsubiri akaweke mafuta, wakamruhusu, alipoondoka hakuonekana tena ukawa ndio mwisho wa Free Mwakangale Jazz.
Wanamuziki wakajikuta wamekwama Mwanza Bahati nzuri baada ya muda mfupi walipata kazi ya kupiga muziki katika bendi moja pale Mwanza, siku moja wakiwa katika bendi hiyo, muwakilishi wa Dar es Salaam Jazz Band , Bi Limi Ally,ambaye alikuwa katika harakati za kumtafuta mpiga gitaa la solo akamsikia Michael Enoch, na ndipo akamuomba ajiunge na kundi la Dar es Salaam Jazz Band. Michael akakubali lakini kusisitiza lazima na wenzake Saiz Vera na Ben Jack wawemo katika bendi hiyo. Baada ya kukatiwa tiketi za treni kwenda Dar es Salaam, muajiri wao wa Mwanza akaleta pingamizi ambalo lilifika mpaka polisi lakini hatimae Michael Enoch na wenzie wakatua Dar es Salaam.

Bendi nyingine ya Mbeya ilikuwa TANU Youth League Jazz Band. Chama cha TANU katika kuelewa umuhimu wa burudani ilianzisha bendi za vijana karibu kila wilaya, na Mbeya haikuachwa nyuma.  Bendi ilirekodi nyimbo kadhaa zikiwemo zilizoimbwa Kilingala!
 Kati ya nyimbo zake zilizokuwa maarufu ni ule ulioitwa Nampenda Firida mwenye macho mazuri.

NAMPENDA FILIDA

Kulikuwa na bendi nyingine ambayo ilisemekana ilitokana na kufa kwa TANU Youth League Jazz Band ilikuwa ikiitwa  bendi ya Lemi au Remi.

AZIMIO CO BANTOU JAZZ YA MBEYA

Bendi nyingine iliyokuweko Mbeya iliitwa Azimio Co Bantou Jazz Band. Kwa wenyeji wa Mbeya wakiangalia vizuri katika picha yao, wataona ilipigwa nje ya nyumba moja ya zilizokuwa kota za wafanyakazi wa  serikali, zilizokaribu na mitaa ya Ghana, pengine hapo ndipo yalikuwa masikani ya bendi hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top