HISTORIA FUPI YA ATOMIC JAZZ BAND YA TANGA

Tanzania yetu ndio nchi ya kusifiwa,
Kote ulimwenguni watu wote watambua,
Tanzania yetu ndio nchi ya furaha
Umaarufu wa wimbo huu umeuwezesha kurekodiwa na wanamuziki vijana wengi na wengine hata kuingia matatani kutokana na kuurekodi bila kupata kibali toka kwa watunzi. Wimbo huu ulirekodiwa na kundi la Atomic Jazz Band mwaka 1967, na mtunzi wake alikuwa Stephen Hiza ambaye bado yupo hai akiendeleza muziki katika mji wa Tanga.
Atomic Jazz Band ilianzishwa mwaka mwaka 1954. Waanzilishi wake Julius Kilua, John Kilua na mwenzao ambae jina la pili limesahaulika aliitwa Dismas, waliita bendi yao Tik Tak Jazz band. Miaka michache baadae, lakini kabla ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, ndipo bendi ilipobadilisha jina na kuitwa Atomic Jazz band. Kama ilivyokuwa wakati ule, bendi iliendeshwa kama klabu, baadhi ya majina ya viongozi wa klabu hiyo, alikuweko mzee ambaye alipewa jina la utani la Mzee Morimori lakini jina lake halisi aliitwa Mze Haji. Baadhi ya wazee wengine wa bendi walikuwa Badi Kidashari, Abdallah Kaungwa na Salim Msema.
Bendi ilikuwa na wanamuziki wenyeji na hata wageni kutoka Kenya na Kongo.
Mmoja wa waimbaji maarufu wa bendi hii miaka ya mwanzoni ya sitini aliitwa Kamaru, inawezekana sana alitoka Kenya. Kamaru alipoacha bendi ghafla mwaka 1965, ndipo walipojiunga vijana wawili waimbaji, Stephen Hizza na Ziggi Said, ambao walitokea kwenye vibendi vidogo vilivyokuwepo Tanga.
Kama ilivyokuwa kawaida miaka hiyo, baada ya kuwa na nyimbo za kutosha, bendi iliingia katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam na kurekodi nyimbo kadhaa zikiwemo Lililokuwa na Mwanzo, Lipi Jema Duniani, na Tanzania Motomoto. Nyimbo zilizoitambulisha kwa wengi Atomic Jazz Band. Na ikaanza kuzunguka mikoa mbalimbali ya Tanznaia n ahata kufanya safari za muziki na kurekodi nchini Kenya.
Walipoingia ten studio mwaka 1967 ndipo uliporekodiwa wimbo maarufu Tanzania Yetu nchi ya Furaha. Nyimbo nyingine zilizorekodiwa zilikuwa ni Leo Nakupasulia, Ewe Hafidha wangu ( wimbo ambao kipande chake cha solo la utangulizi kilichukuliwa na kampuni moja ya sinema ya Norway na kuwa sehemu ya ‘sound track ya filamu yao).  Wakati huo wanamuziki waliokuwa katika bendi walikuwa niJohn Mbula-Saxophone, John Kilua- Conga, Gislan Dejean (Mkongo) kwenye gitaa la bezi, Harrison Siwale kwenye gitaa la ridhim,  Hassan Ngoma –solo gitaa.
Kama ilivyokuwa kawaida ya bendi nyakati zile, wanamuziki walihama bendi kutoka bendi moja kwenda nyingine, kwa sababu mbalimbali, zikiwemo maslahi na mara nyingine kuongeza ujuzi au kupiga katika bendi ambayo mwanamuziki aliona inapiga muziki inaoutaka.Billy Mbwana, Harrison Siwale Hassan Ngoma na Twaha Shabani waliihama bendi kwa nyakati tofauti. Nafasi zao zikajazwa na wanamuziki wengine kama Rodgers Isaac, John Kijiko, Mohamed Mgoro na Mganga Hemed. Katika awamu ambayo John kijiko alijiunga na Atomic Jazz Band, nyimbo ambazo bado zinakumbukwa mpaka leo zilirekodiwa. Nakujutia Salima, Lina, Mado Mpenzi( wimbo huu ulisajiliwa kama utunzi wa John Kijiko, lakini ulikuwa utunzi wa kijana mwanafunzi ambaye alitaka kuwa  mwanamuziki lakini wazazi wake walikataza asishuhulike na muziki, mpaka leo mtunzi huyo hujulikana kwa jina la Mado kwa rafiki zake).
Mwaka 1977 na 1978 ulikuwa wa mikiki mingi kwa Atomic Jazz Band, wanamuziki kadhaa wakaiacha band, Mganga Hemedi akajiunga na Urafiki Jazz Band, John Mbula, John kijiko, na Rodger Isaac walahamia UDA Jazz Band. Mohamed Mgoro alihamia Polisi Jazz Band. Huo ukawa mwanzo wa mwisho wa Atomic Jazz Band. Mpiga gitaa Patrick Kamale alivaa viatu vya John Kijiko mpaka bendi ilivyopotea katika anga za muziki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top