Nataka kuanzia leo niwazungushe mikoa mbalimbali ambako kulikuwa na bendi. Bendi nyingine zilikuwa maarufu mpaka kujulikana nje ya nchi yetu na nyingine hazikuwa maarufu au hazikudumu sana, lakini kuna wasanii wengi waliotoka kwenye bendi hizo ndogo na kuja kuwa maarufu nchini na hata duniani.
Nianze na Kigoma, huu si mji ambao siku hizi unatajwa wakati ukiongelea muziki wa dansi lakini kulikuwa na bendi kadhaa kutoka mji huo zilizokuja kujitokeza, tuanze na Lake Tanganyika Jazz Band, wenyeji waliita tu Lake Jazz, hii ndiyo bendi alikotokea mpiga solo, mtunzi na muimbaji Shem Karenga,. Shem alianza muziki huko akiwa mpiga gitaa la bezi na hatimae kuhamia Tabora jazz band ambako nyota yake iling’ara akiwa mpiga gitaa la solo. Hapa nigusie kitu, kuna wapiga gitaa la solo wengi ambao hatimae walikuja kuwa wapiga gitaa maarufu, nani hamkumbuki Joseph Mulenga, mpiga bazz wa Dar es Salaam International Orchestra aliyekuja kuwa mpiga solo maarufu wa Mlimani Park, Bima Lee, Legho Stars na MK Group?.
Kigoma pia kulikuweko na bendi iliyoitwa Super Kibisa Jazz Band, bendi hii ilikuwa na waimbaji wazuri na wapigaji wazuri sana, mmoja wa wapiga magitaa wa bendi hiyo Mzee Simba, hatimae alikuja kujiunga na JKT Kimbunga, bendi aliyokaa nayo mpaka alipostaafu. Pia kulikuweko na bendi iliyochukua jina la mji huo na kuitwa Kigoma jazz band, bendi nyingine iliyokuweko Kigoma iliitwa Kasababo Jazz Band, hii ndiyo ilikuwa kati ya bendi za awali kabisa ya marehemu Shaaban Dede.
Mkoa jirani wa Mara ulikuwa na bendi nyingi pia, bila shaka ni vizuri kuanza na bendi ya Mara Jazz Band, hii ilipata umaarufu mkubwa ikiwa na mtindo wake wa Sensera. Lakini pia kulikuwa na bendi iliyochukua jina la mji wa Musoma, bendi iliyoitwa Musoma Jazz Band hii ilijitambulisha kwa mtindo wake wa Segese. Bendi nyingine kutoka mkoa huu ilikuwa Special Baruti Band, hii ndiyo bendi ya awali ya muimbaji maarufu Jerry Nashon kabla hajaingia jiji la Dar es Salaam. Musoma kulikuwa na bendi iliyokuwa mali ya Kanisa Katoliki iliyoitwa Juja Jazz, kulikuweko na bendi kadhaa nchini ambazo ailikuwa chini ya kanisa Katoliki, hata kule Iringa kulikuwa na bendi nyingine mali ya Kanisa katoliki iliyoitwa VICO Stars ikiwa ni kifupi cha Vijana Consolata Stars, bendi hizi hazikupata umaarufu kwani zilikuwa zikipiga katika maeneo ya kanisa au kwenye sherehe za kikanisa tu. Bendi nyingine kutoka mkoa wa Mara ilikuwa ni Eleven Stars Band, japo ilijiita jina hilo, bendi ilikuwa na wanamuziki sita tu.
Tukiingia jiji la Mwanza, jiji lililokuwa likijisifu kwa starehe miaka ya sitini na sabini, kutokana na almasi, pamba na biashara ya mifugo, wenyewe walikuwa wakijisifu na kusema juu mali chini mali yaani juu kuna ng’ombe na chini kuna almasi. Mwanza kulikuwa na bendi kadhaa ikiwemo Kimbo Twist Band ambako waliwahi kupita kati ya wapiga solo mahiri waliowahi kutokea Tanzania, marehemu Rashid Hanzuruni na marehemu Kassim Mponda. Mwanza pia kulikuwa na bendi ambayo asilimia kubwa walikuwa ni wanamuziki kutoka Kongo, bendi hiyo iliitwa Orchestra Super Veya, bendi hii ilikuwa na umaarufu mkubwa kanda ya ziwa na ndiko alikopitia mwanamuziki maarufu Mzee Zahir Ally Zollo.

Mji wa Shinyanga kulikuwa na bendi maarufu iliyoitwa Shinyanga Jazz Band, bendi hii ilirekodi nyimbo kadhaa lakini wimbo wao mmoja unakumbukwa na wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo unaitwa Tenda Wema nenda zako. Wimbo huu ulitungwa na marehemu Zacharia Daniel Mabula, na kwa sababu ya wimbo huo mpaka kifo chake mtunzi aliitwa Zacharia Tendawema au Mzee Tendawema. Nae alitengeneza historia yake ya muziki kwa kupitia bendi nyingi maarufu zikiwemo Western Jazz Band, JKT Kimulimuli na TANCUT Almasi Orchestra ambako pia huko alitunga nyimbo nyingi, lakini wimbo wa Tenda wema nenda zako ulikuwa ndio nembo yake mpaka alipofariki.
Tabora ulikuwa mji uliochangamka sana, kwanza ni moja kati ya miji ya zamani sana nchini, pili Tabora ulikuwa mji wenye vijana wengi kutokana na kuwa na shule na vyuo vilivyokuweko katika mji ule. Kulikuwa na shule kongwe kama Sekondari ya Tabora Boys na Sekondari ya Tabora Girls, pia vyuo kama Tabora Secretarial, chuo cha Ualimu cha Tabora, na chuo kikongwe cha reli, Railway Training School. Hivyo basi Tabora nayo ilichangamka sana kimuziki, kulikuwa na bendi maarufu ya Tabora Jazz Band, na bendi yake dada, Nyanyembe Jazz band na pia ilikuweko bendi kongwe ya Kiko Kids. Wanamuziki wengi sana maarufu walitoka bendi hizi wakiwemo Shem Karenga , Wema Abdallah, Kassim Karuona na Salum Zahoro, majina yaliyokuja kuvuma Afrika ya Mashariki na kati.

Mwaka 1972 Mzee Moses Nnauye aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Singida, kutokana na kupenda kwake muziki haikuchukua muda mrefu akahakikisha Singida ikapata bendi nzuri iliyoitwa Ujamaa Jazz Band, bendi iliyokuwa ikipiga kwa mtindo iliyouita King’ita Ngoma. Wanamuziki kadhaa kama Waziri Ally, Selemani Mwanyiro walipitia bendi hii. Nikumbushe jambo jingine kuwa Mzee Nnauye alipokuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo pia alianzisha bendi iliyoitwa Sabasaba Jazz band, mtindo wa bendi hiyo uliitwa Kizibo. Moses Nnauye alimualika kwanza Mzee Nyange aliyekuwa mpiga solo wa Cuban Marimba kujiunga na Sabasaba Jazz Band , Nyange alipokataa Hamza Kalala aliyekuwa nae mwanamuziki wa Cuban Marimba akakubali wito ule na kujiunga na Sabsaba Jazz Band

Mwaka 1948 Uingereza iliigawa nchi katika majimbo manane na Dodoma ikawa katika jimbo lililoitwa Central Province (Jimbo la Kati), na pia Dodoma iko katikati ya nchi hivyo basi wanamuziki kadhaa walianzisha bendi yao wakaiita Central Jazz band, wimbo wao maarufu ulikuwa Dada twende tukalime tukajenge nchi yetu.
Bendi nyingine iliitwa the Jolly Sextet Band. Bendi hii ilianzishwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa Shirika la Posta la Afrika ya Mashariki, wakati huo likijulikana kama East African Posts and Telecommunications Corporation (EAPTC). Mkenya huyu alikuja na vyombo vyake vya muziki na kati ya watu walikuja kuwa maarufu waliotokea bendi hiyo ni mpiga saksafoni maarufu Mnenge Ramadhani aliyekuja kupata umaarufu mkubwa alipokuwa JUWATA Jazz band. Mfanya biashara mmoja, Mohamed Omar Badwel, aliyekuwa na gereji na studio ya kupiga picha alinunua vyombo na kuanzisha bendi iliyokuja kuitwa Dodoma Jazz Band. Bendi hii ilikuwa na wanamuziki wazuri sana na ilitoa nyimbo zilizokuja kufahamika nchi nzima. Mmoja kati ya wapiga solo wa kwanza wa bendi hii alikuwa Hassan Mursali kwa asili alikuwa Mnyasa, baadae alihamia NUTA Jazz Band na solo lake linasikika katika ule wimbo maarufu wa Dunia Njema.
Kabla hatujaondoka mkoa wa Dodoma tuumalize kwa kuitaja bendi nyingine maarufu iliyotoka wilaya ya Mpwapwa na ikaitwa Mpwapwa Jazz Band. Bendi hii haikuwa ndogo kwani iliweza kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilipata umaarufu wa Kitaifa wakati wa uhai wake, ikiwemo wimbo Nilikuwa sina kazi.
Kutoka Dodoma tunaingia mkoa wa Iringa, na kuingia mji wa Iringa, ambao ulianza hasa kama ngome ya Wajerumani walipokuwa katika harakati za kumsaka Mutwa Mkwawa, baada ya kuangusha ngome yake kule Kalenga. Jeshi la Wajerumani likiwa na maafisa wachache wa Kijerumani, lilikuwa na askari wengi wa Kiafrika kutoka pande mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kati. Kulikuwa na askari wa Kinubi, askari wa Kimanyema, askari wa Kizaramo, askari wa Kinyamwezi na makabila mengine kadha wa kadha. Askari hawa wakaanza kuishi na familia zao maeneo yanayojulikana kama Miyomboni, jirani na kituo kikuu cha polisi ambapo haswa ndipo yalikuwa makao makuu ya jeshi la Wajerumani.
Watoto na wajukuu wa askari hawa walikuwa wakijitambulisha kuwa wao ndio wenyeji halali wa mji wa Iringa. Walijiita Born Town. Hivyo walikuwa na timu ya mpira iliyoitwa Boni kifupi cha Born Town. Na pia wakaanzisha pia bendi iliyoitwa Boni Jazz band, pengine moja kati ya bendi za awali za mji huu. Kama ilivyokuwa Dodoma kuwa na bendi inaitwa Sextet Jazz band, Iringa kulikuwa na bendi inaitwa Habanero Jazz Band. Sextet na Habanero yalikuwa majina ya bendi mbili za huko Cuba. Katika zama hizo bendi za hapa nchini zilikuwa zikiiga muziki kutoka Cuba, si Congo, hivyo na majina ya bendi zao yalikuwa yaKispanyola. Bendi ya Iringa iliyokuja kupata umaarufu mkubwa ilikuwa Highland Stars Band. Mpiga gitaa Abel Balthazar ni moja ya wapigaji maarufu waliowahi kupitia bendi hii. Nyumbani kwa mpiga solo maarufu wa Msondo Ngoma Ridhwani Abdul Pangamawe, ndipo yalipokuwa yakifanyika mazoezi ya Highland Stars Band. Baba yake na mama yake Ridhwani wote walikuwa wakijua kupiga magitaa, si ajabu kabisa nyumba hiyo kutoa mpiga gitaa na kinanda mahiri anayetingisha nchi mpaka leo. Moja ya wimbo wao maarufu wa Highland Stars ulikuwa ni Sitasita Mpenzi.

Kwa vile nimetokea mji wa Iringa nakumbuka kitu kimoja ambacho hakipo tena leo. Zama hizo hakukuweko na matangazo ya kubandika karatasi wa vipaza sauti, hivyo basi siku ambayo bendi ilikuwa inataka kupiga, bendi nzima ilijipanga nyuma ya pickup na kufunga vyomb na kuanza kupita mitaani huku wakiwa wanapiga muziki ‘live’. Na hapo hapo kutangaza ukumbi gani watakuwepo na kiingilio husika.
Bendi nyingine mjini Iringa ilikuwa ni Iringa Jazz Band, hii ilikuwa mali ya tawi vijana wa TANU au TANU Youth League. Miji mingi sana ilikuwa na bendi za TANU Youth League katika miaka ya 60 na 70.
Mkwawa High School, ambayo awali ilikuwa shule ya ‘Wazungu’ na iliyokuwa ikiitwa St George and St Michael European School, ilikuja kuwa na bendi nzuri sana ya wanafunzi iliyoitwa Orchestra Mkwawa. Wakiwa na mtindo wao waliouita Ligija walitoa burudani kila mwisho wa wiki katika ukumbi wa Welfare Center, katika utaratibu wa madansi ya mchana maarufu kama Buggy, wao kama wanafunzi hawakuwa na ruksa ya kuwa katika kumbi za dansi usiku, hivyo waliweza kupiga muziki huo mchana tu. Pia katika shule hiyo hiyo kulikuwa na bendi nyingine iliyokuwa ikipiga muziki wa Kizungu na iliitwa Midnight Movers. Marehemu Eddy Hanspoppe, Deo Ishengoma na Martin Mhando walikuwa kati ya wanamuziki wa bendi hii. Vyombo walivyotumia vilikuwa ni vile ambavyo vilikuwa vikitumiwa na bendi iliyokuwa ya TANU Youth League ya Iringa.
Magitaa ya bendi hii hatimae yalikuja kuchukuliwa na vijana wachache, mimi nikiwa mmoja wao, walioanzisha bendi iliyokuja kujulikana kama Chikwalachikwala. Chikwalachikwala ikajigawa na ikaanzishwa bendi iliyoitwa BOSE Ngoma, jina lililotokana na aina ya speaker walizokuwa nazo.
Mwaka 1986 ikazaliwa Tancut Almasi Orchestra bendi nyingine kubwa iliyowahi kutokea Iringa, bendi hii ilikuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Diamond Cutting Company kilichokuwa pale Iringa. Majina ya wanamuziki maarufu waliopitia bendi hii ni mengi sana kati hao walikuweko mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Banza Tax, Mafumu Bilali, Kawelee Mutimwana, Shaban Yohana Wanted, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Dingituka Molay, Amani Ngenzi, Joihn Kitime na wengine wengi.
Bendi nyingine iliyowahi kuweko Iringa mjini ni Ruaha International Orchestra , iliyokuwa mali ya mfanya biashara mmoja aliyeitwa Batista Mtandi. Bendi hii ilikuwa chini ya uongozi wa muimbaji marehemu Kalala Mbwebwe, aliyehamia huko baada ya kuvunjika kwa bendi yake ya awali ya Tancut Almasi Orchestra, na wimbo wake Lutadila ni kumbukumbu kubwa kwa wapenzi wa bendi hii.

Bendi nyingine zilizowahi kuwa Iringa, zilikuwa ni VICO Stars,(Vijana Consolata Stars) iliyokuwa mali ya kanisa Katoliki, Living Light Band iliyokuwa mali ya hoteli ya Living Light.
Kumaliza mkoa huu bila kutaja bendi maarufu ya JKT Mafinga haitakuwa sawa. Bendi hii ilikuwa maarufu kwa jina la Kimulimuli, jina hili lilitokana na taa za disco zilizokuwa zinafungwa wakati bendi hii inapiga. Vyombo maarufu vya muziki aina ya Ranger FBT ambavyo vilikuwa vikitumika na bendi nyingi miaka ya 80 vilikuwa vinakuja na taa za disco (kimulimuli), na wenyeji wa Mafinga walikuwa wakisema kwa Kihehe ‘Twibita kukina kimulimuli’ yaani tunaenda kucheza Kimulimuli, na hakika jina hilo ndilo likawa utambulisho wa bendi hiyo, na hata bendi yenyewe ilitunga nyimbo kusifia jina lao la Kimulimuli. Kati ya wanamuziki maarufu waliowahi kupitia bendi hii ni Zahiri Ally Zorro na Zakaria Daniel Mabula Tendawema ambaye nimeelezea jinsi alivyopata jina la Tendawema……….safari inaendelea
