Muziki wa Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika umepitia katika milima na mabonde mengi sana, jambo ambalo ni kawaida kwa sanaa za aina zote. Hakuna shaka kabisa kuwa wanasiasa katika nchi yetu nao wamechangia sana katika kuufikisha muziki wetu hapa ulipo. Nina hakika kuna jambo la kujifunza kwa wanasiasa wa sasa jinsi tamko la kawaida linavyoweza kutengeneza historia mpya.
Hebu turudi nyuma na kuzungumzia muziki wa vijana wa miaka ya 60 na 70, na hasa muziki ule ambao haukuwa na muelekeo wa rumba, na tuone jinsi tamko la kisiasa lilivyougusa na matokeo yake katika historia ya muziki na wanamuziki wa nchi yetu.
Miaka hiyo ya 60 na 70na hata 80, vijana wanamuziki waliokuwa shule za sekondari walitengeneza bendi zao. Na bendi nyingi kati ya hizi, zilipiga muziki wake kwa kuiga muziki wa mahadhi ya nchi za Magharibi, na hasa zilizokuwa zinazungumza Kiingereza. Wanamuziki hawa walikuwa wakipiga muziki wao kwa kuiga na kupiga nyimbo za vikundi na wanamuziki maarufu wa Ulaya na Marekani, kama vile The Beatles, The Temptations, The Famous Flames, Jimi Hendrix Experience na kadhalika. Hata majina ya vikundi vyao yaliigwa kutoka hukohuko Magharibi, kama ilivyokuwa kwa wenzao ambao walikuwa wakipiga muziki wa rumba walivyofanya. Wakati vikundi vya muziki wa rumba vikijipa majina yaliyokuwa na utambulisho wa Jazz Band au Orchestra kwa mfano, Western Jazz Band, Kilwa Jazz band, Orchestra Selesele, Orchestra Santa Fe na kadhalika, vikundi hivi vyenye mtizamo wa Kimagharibi vilikuwa na majina ya Kiingereza yasiyo na kisifa cha jazz band au orchestra kwa mfano, The Sunburst, The Comets, The Rifters, The Jets, The Barkeys, The Barlocks The Hot Fives, The Sparks, The Tonics, The Flames, The LoveBugs, The Revolutions na kadhalika. Hata bendi za dansi ziilizoanzia mfumo huo wa kupiga muziki wa Kimagharibi lakini baadae kuanza kupiga rumba, nyingi zilibaki na sifa hiyo ya kutojiita Jazz band, kama vile Safari Trippers, Afro 70, Alfa Afrika na kadhalika
Miji ambayo ilikuwa na bendi nyingi za muziki wa hadhi ya Kimagharibi ilikuwa ni Dar es Salaam, Tanga na Arusha. Wakati wa kuzungumzia muziki huu huwezi kuacha mchango wa bendi zilizoanzishwa na vijana wa Kigoa. Hawa asili yao ilikuwa Bara Hindi, lakini wao huzungumza Kiingereza na wengi ni waumini wa Kikristo. Hawa nao walikuwa na bendi zao karibu kila mji walipokuwepo. Bendi ya The Kilimanjaro, maarufu kama Wananjenje, historia yao ilianza kutokana na bendi ya The Love Bugs iliyoanzishwa na vijana wa Kigoa wakazi wa jiji la Tanga. Bendi ya Barlocks ya Dar es Salaam ilianzishwa na vijana wa Kigoa wa Dar es Salaam, pia kulikuweko na George De Souza Band, The Demellos na kadhalika.

Kituo cha Utamaduni cha Marekani kilichojulikana kama United States Information Service (USIS), ambacho kilikuwa jirani na ukumbi wa sinema wa Empress, nacho kilichangia sana kwa vijana wa wakati huo kupenda muziki na utamaduni wa Kimarekani. Katika kituo kile kulikuwa na sinema mara kwa mara zikionyesha wanamuziki wa Kimarekani, palikuwa na santuri za nyimbo za Kimarekani za kuazima na hata za kusikiliza palepale kituoni. Pia kulikuwa na magazeti kama the Ebony, yaliyokuwa yakionyesha maisha ya wasanii na wanamichezo weusi wa Marekani. Kubwa zaidi kituo kilikuwa kikileta wanamuziki ambao wakati huo walikuwa na sifa kubwa duniani, na wanamuziki hao wakafanya maonyesho ya bure viwanja vya Mnazi Mmoja. Kati ya wanamuziki ninaowakumbuka waliowahi kufanya maonyesho nchini ni mpiga gitaa Buddy Guy na kundi lake, na pia kundi la Staple Singers. Uwanja wa Mnazi Mmoja wakati huo ulikuwa uwanja wa burudani kwa wakazi wa Dar es Salaam. Kulijengwa jukwaa ambalo lilikuwa likitumika karibu kila mwisho wa wiki kwa burudani, ndani ya uwanja wa Mnazi Mmoja kulikuwa na baa ambayo ilikuwa wazi kila siku, kilikuwa kiwanja cha umma haswa. Huyu Buddy Guy alikuwa mmoja wa wanamuziki aliyeamsha ari ya upenzi wa muziki wa ‘soul’. Vijana wakaupenda sana muziki huu. Majina makubwa ya wanamuziki wa soul wakati huo na nyimbo zao zilikuwa midomoni mwa vijana wapenda muziki wa aina ile. Otis Redding, Wilson Pickett, Isaac Hayes, James Brown, Aretha Franklin na bila kumsahahu Clarence Carter.
Kutokana na maadili ya wakati ule, vijana walioko shule hata kama ni wa sekondari hawakutakiwa kuwa madansini usiku, hivyo basi kukaanzishwa utaratibu wa muziki ulioitwa Bugi,muziki huu wa vijana ulikuwa maarufu siku za Jumamosi na Jumapili na siku za sikukuu mchana kuanzia saa 8 mpaka saa 12 jioni. Shule nyingi zilikuwa zinaruhusu Bugi kwenye kumbi za shule. Hata shule za madhehebu ya dini kama vile Salvatorian School, ambayo baadae ilikuja kuwa St Joseph Primary School, ilikuwa inaruhusu bendi za vijana kupiga kamuziki katika maeneo ya shule siku za mwisho wa wiki.
Mara ya mwisho nimehudhuria bugi pale ilikuwa mwaka 1973, vijana wa Comets walikuwa walipiga siku hiyo, na bado ninakumbuka nyimbo mbili zilizopigwa pale, Mammy Blue wa bendi ya Pop Tops na Alobe wa Negro Success. Kiingilio kilikuwa kiasi cha senti thelathini.

Ni wakati wa enzi za muziki huu kukazaliwa aina mpya ya muziki iliyokuwa ikiitwa Afro Rock, mchanganyiko wa muziki wa Rock na muziki wa Kiafrika. Bendi ya Osibisa, iliyokuwa na mchanganyiko wa wanamuziki kutoka nchi mbalimbali za Afrika na mwanamuziki Fela Anikulapo Kuti kutoka Nigeria walikuwa baadhi ya wanamuziki walioweza kuutambulisha muziki huu mpya duniani.
Afro Rock ilikuwa pana sana, kwani wanamuziki kutoka kila kona ya Afrika walianza kutumia muziki wao wa kiasili na kuchanganya na rock na kuja na aina yao ya muziki, kwa mfano Patrick Balisidya na Afro 70 walikuja na mchanganyiko wao wa muziki wa Kigogo na rock, Jets wakawa na nyimbo yao moja ya Kizaramo na Rock, Mulemuleme, bendi ya The Sparks wakaja na wimbo wao wa Kizaramo pia Nofa na Nzala. Huu wimbo wa Nofa na Nzala umefufuka baada ya kurekodiwa tena wiki mbili zilizopita na mwanamuziki wa Afrika ya Kusini aitwae Vulindlela Yeni. Vuli alikuwa mmoja ya vijana waliokimbia kwao kutokana na siasa za ubaguzi zilizokithiri Afrika ya Kusini wakati huo.
Vuli alikuwa mpiga saksafon na hivyo kupigia bendi nyingi za hapa ikiwemo Boma Liwanza, Rifters na Safari Trippers, hatimae alikuja kuwa mmoja wa wanamuziki wa kundi la Lucky Dube, na ndie aliyekuwa mwalimu wa mpiga saksafon maarufu Akuliake Salee maarufu kama King Maluu.
Bendi ya Sunburst nayo ilikuwa na nyimbo za Kiswahili katika mtindo wa Afro Rock, nyimbo zao kama Kosa langu nini, Simba anaunguruma na kadhalika zilikuwa maarufu na kuwapa ushindi wa Bendi Bora mwaka 1973. Katika zama hizo kila nchi katika Afrika ikaingia katika mchuano wa kuleta aina yake ya muziki wa Afro Rock, na kuanza kuiweka Afrika katika ramani ya muziki duniani.

Kwa bahati mbaya bendi hizi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wenye mlengo wa magharibi hazikuwa maarufu kwa kurekodi nyimbo zao, hivyo picha na hadithi zao tu ndio zimebaki, lakini zile chache ambazo zilirekodi zimeacha alama kubwa ya kudumu ambayo bado inaheshimika. Kati ya bendi zilizorekodi nyimbo nyingi kwa mtindo wa Afro Rock wakati huo ni Afro 70 na Sunburst. Miaka michache iliyopita kampuni ya Strut Records ilisambaza upya nyimbo za bendi ya Sunburst. Patrick Balisidya wakati wa uhai wake aliwahi kurekodi upya nyimbo za Afro 70 akiwa na kundi la Archimedes Badkar la huko Sweden

Jambo la kusikitisha ni kuwa wakati wanamuziki wa Afrika nzima wakijitahidi kupata nafasi ya ‘kutoka’ na kuwa kwenye ramani ya muziki duniani miaka hiyo, tarehe 12 Novemba mwaka 1969 ulifanyika mkutano kati ya waalimu na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dar es Salaam ilikuwa sehemu ya mkoa wa Pwani wakati huo. Katika mkutano huo waalimu wa shule za sekondari walilalamika kuwa wanafunzi wao wanaharibika kutokana na muziki wa ‘soul’. Hapa ulikuwa unajumuishwa muziki wote wenye hadhi ya Kimagharibi ambao ulikuwa ukipendwa na vijana wakati huo. Baada ya mkutano huo, kupitia gazeti la Standard, Mkuu wa Mkoa akatoa amri ya kupiga marufuku muziki huo katika mkoa wake. Mkoa ambao ulikuwa ndio wenye shughuli nyingi na wanamuziki wengi wa muziki wa Afro Rock, tamko hili likauwa ushindani wa wanamuziki wa Afro Rock wa Tanzania. Bado najiuliza kama tamko lile lisingetoka wanamuziki wa Tanzania wangetoa mchango gani katika muziki wa Afro Rock?

Fantastic Bro don’t forget the Brother of George, Robert (Robby)+de’Souza He passend away Long ago na George yupo Canada ndiko anaishi sasa.
Mzee Nick, true George De Souza niliwasiliana nae akanitumia picha nyingi za magazeti, nitaitoa stori yake humu si muda mrefu