Katika aina ya muziki unapotea ni muziki wa gitaa baridi unaopigwa na mtu mmoja. Gitaa baridi ni gitaa lisilotumia umeme, wengine huliita Galaton au kwa Kiingereza huitwa Acoustic guitar. Chombo hiki husemekana kiliingizwa Afrika kwa mara ya kwanza na mabaharia wa kutoka Ureno katika karne ya 15, Toka wakati huo Waafrika kutoka pande mbalimbali za bara hili, wameweza kutafuta njia tofauti za kulipiga gitaa. Tafiti zinaonyesha staili mbalimbali za upigaji wa chombo hiki unatokana na wanamuziki kupiga gitaa kwa kuiga vyombo vyao asili. Mfano staili za upigaji wa gitaa kavu wa baadhi ya wapigaji kutoka Afrika Magharibi, umetokana na kujaribu kulipiga gitaa kwa mtindo wao wa kupiga chombo chao asili cha muziki kiitwacho Kora. Tukirudi hapa kwetu, upigaji wa magitaa umekuwa unatafsiri vyombo kama Litungu, kalimba na vyombo mbalimbali vya asili ambavyo hupigwa kwa kudonoa donoa.
Muziki wa mtu mmoja kupiga gitaa baridi ulikuwa maarufu sana miaka ya 50 na 60, na walikuweko wanamuziki maarufu sana wa staili hiyo ya upigaji. Tupate historia fupi fupi za baadhi ya wapigaji hawa. Tuanze na mmoja wa wapigaji maarufu kutoka Tanganyika, huyu alikuwa marehemu Frank Joseph Humplick, Frank aliunda kundi la wanamuziki ambalo yeyey alikuwa akipiga gitaa na dada zake wakawa wanamsindikiza kuimba, kundi hili aliliita, ‘Frank na Dada zake’. Kundi hili lilikuja kuwa maarufu sana Afrika ya Mashariki.
Baba yao alitoka Austria na mama yao alikuwa Mchaga, Frank akiwa mtoto wa pili kuzaliwa, alizaliwa tarehe 3 April 1927 na kufariki tarehe 25 Agosti 2007. Wakati wa ujana wake alijulikana kama ‘Chaga Boy’ kutokana na kuwa na tabia ya kuzurula kila mahala na gitaa lake mgongoni.
Upigaji gitaa wa Frank ulikuwa ni mchanganyiko wa upigaji wa muziki wa zamani wa Kimarekani wa Country western na ubunifu wake binafsi. Wimbo maarufu kuliko wote wa kundi hili ulikuwa ni Harusi, kwa vile ulikuwa haukosekana kupigwa kwenye harusi ulijulikana kama wimbo wa Harusi wa Afrika Mashariki.

Kati ya wapigaji wengi sana wa gitaa baridi nchini Kenya, alikuweko marehemu George Mukabi. Mwanamuziki huyu alikuja kuuwawa na shemeji na wakwe zake kutokana na ugomvi ulioanza mke wake alipoangusha gitaa lake mara baada ya yeye kutoka kurekodi. Upigaji wa George Mukabi ulikuwa ukiiga kabisa muziki wa kabila lake na ulikuwa tofauti kabisa na ule wa Frank Humplick.
Mwaka 1930 katika iliyoitwa Belgian Congo ambayo sasa ndiyo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, katika kijiji cha Bunkenya kilichopo jimbo la Lualaba, alizaliwa mtoto aliyepewa jina la John Bosco (Jean Bosco). Maisha yake ya awali aliishi Lubumbashi ambako alikuwa maarufu kwa kupiga gitaa lake jioni wakati mchana akiwa mfanyakazi wa benki. John Bosco ambaye pia alijiita Mwenda wa Bayeke kutokana na utaratibu ulizoanzishwa na Rais Mobuto wa Kongo wa kuwahamasisha wananchi wake kutumia majina ya kiasili, alikuwa akipiga gitaa lake kwa kuiga upigaji wa kalimba wa kabila la Waluba. John Mwenda Bosco alifariki katika ajali nchini Zambia mwezi Septemba, mwaka 1990. Mkongo mwingine aliyekuwa bingwa wa muziki wa gitaa la mtu mmoja alikuwa Losta Abelo. Abelo alikuwa rafiki wa John Mwenda Bosco, lakini upigaji wake wa gitaa ulikuwa wa aina yake tofauti kidogo na John Mwenda Bosco. Losta Abelo alikuwa maarufu sana Afrika ya Mashariki pia kwa sababu kama aliimba nyimbo nyingi sana kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya nyimbo zake bado zinapigwa na bendi kadhaa hata hapa nchini Tanzania mpaka leo.
Mpiga gitaa mwingine maarufu kutoka Kongo aliitwa Edward Masengo. Edward alikuwa binamu yake John Mwenda Bosco ambaye upigaji wake wa gitaa nao ulikuwa tofauti na wenzake.
Edward Katiti Masengo alizaliwa Kafubu katika jimbo la Katanga mwaka 1933. Mwaka 1950 Masengo alikwisha hamia Kenya na kuanza shughuli za sanaa huko,alikwa na kundi la vichekesho na dansa, na ni wakati huo aliwaunganisha John Mwenda Bosco na Peter Colmore ambaye alikuwa na kampuni maarufu ya matangazo ya Andrew Crawford Production, lakini wakati huo alikuwa bado anaishi Lubumbashi. Mwaka 1960 akahamia rasmi Kenya, ambako alipata umaarufu mkubwa kutokana na upigaji na sauti yake kusikika katika matangazo mengi ya bidhaa za Kenya, aliweza kurekodi hata na Miriam Miriam Makeba na Harry Belafonte. Mwaka 1972 Masengo alirudi Lubumbashi lakini kwa sababu ambazo hazijulikani, serikali ya wakati ule ikamnyang’anya mali zote na Masengo akafariki masikini tarehe 27 Machi 2003.
Wapiga magitaa wengi sana Tanganyika walianza kuiga upigaji wa JohnMwenda Bosco, kwa mfano wimbo maarufu wa Salamu za Wagonjwa uliopigwa na marehemu Omari Kungubaya ni mfano wa jinsi wapiga magitaa walivyoiga upigaji wa John Mwenda Bosco.
Upigaji wa magitaa wa staili ya mtu mmoja,mara nyingine ukisindikizwa na mtu aliyegonga chupa au chuma, ulikuwa maarufu sana vijijini kila upande wan chi, na wapigaji walikuwa na tungo zilizokuwa zikielezea haswa maisha katika sehemu walizokuwa. Watu wa Iringa hakika watamkumbuka Mzee Chavalikungu aliyekuwa mpigaji mzuri sana wa gitaa kavu na nyimbo zake zilikuwa zinachekesha zenye mafunzo zilihusu maisha ya kawaida ya kijiji cha Uheheni.
Tarehe 16 June 1932, pale kijijini Tosamaganga Iringa, alizaliwa mvulana akapewa jina la Francis Raphael, baba yake Raphael Kitime alikuwa mwalimu wa Tabora School, mama yake Elizabeth Saula pia alikuwa na taaluma ya ualimu. Alipofika darasa la nne tayari alikuwa katika bendi ya shule akipiga tarumbeta. Baadae akaja kujifunza kupiga vyombo vingine kadhaa vikiweko, banjo, accordion, saxophone na gitaa. Francis alilazimika kujiunga na shule ya wavulana ya Tosamaganga iliyokuwa na mabweni. Francis nae alikuja na aina yake ya upigaji wa gitaa uliofuata mirindimo ya nyimbo za kabila lake la Kihehe. Francis alirekodi baadhi ya nyimbo zake kwa mara ya kwanza kwenye studio za Tanganyika Broadcasting Corporation mwaka 1959. Mwaka 1994 mwanae John Kitime alirekodi nyimbo 13, katika nyimbo 3 mke wake Christina Kitime pia alishiriki, kanda za nyimbo hizo zilianz kusambazwa na kampuni na RetroAfric mwaka 1996.
pic

Mpiga gitaa kavu mwingine maarufu alikuwa John Ondolo Chacha, yeye alizaliwa mwezi Machi mwaka 1917 katika kijiji cha Kirumi wilaya ya Musoma. Kwa kabila alikuwa Mkurya. Kutokana na jina lake la Chacha, ni wazi alikuwa mtoto wa kwanza kuzaliwa. Baba yake aliitwa Joas Aliongo Mwaka na mama yake aliitwa Norah Alionga Muroka. Miaka michache baada ya wazazi wake kuoana wakaamua kuhamia Kenya kutafuta maisha, wakati huo Afrika ya Mashariki ilikuwa kama nchi moja kwa vile eneo lote lilikuwa chini ya utawala wa Uingereza, hivyo kulikuwa hakuna haja ya passport wala vibali vyovyote kuhama toka sehemu moja kwenda nyingine.
Baada ya familia kuhamia Kenya, Mzee Joas akapata kazi katika shamba la chai lililoitwa Majani Mingi, John Ondolo akaanza masomo katika shule ya msingi ya kimisionari ya Mukumu iliyokuwepo Kakamega.
Mwaka 1928 familia hiyo ikahamia Nairobi na John Ondolo akajiunga na shule ya St Peter Claver. Hii ilikuwa shule ya wamisionari Wakatoliki. St Peter Claver ilifunguliwa mwaka 1923 na inasemekana ndio ilikuwa shule ya kwanza Kenya iliyokuwa na wanafunzi wa makabila mchanganyiko.
John Ondolo alipokuwa shule hii ndipo kipaji chake kilianza kugundulika, alijifunza kupiga gitaa, piano na vyombo vingine. Bahati mbaya uwezo wa wazazi wake ukawa mdogo wakashindwa kuhimili ada ya shule hii hivyo akafukuzwa shule.
Mwaka 1942 John Ondolo alijiunga na jeshi la Waingereza, lililoitwa King’s African Rifles kwa kifupi KAR, watu wa kawaida waliwaita askari wa jeshi hilo askari Kea. Alipokuwa jeshini ndipo akagundulika kuwa pia anakipaji kikubwa cha kuchora, kipaji hiki kilifanya hata atambuliwe na malkia wa Uingereza kwa kazi hiyo. Mwaka 1947 aliacha jeshi na mwaka 1948 akaanza kufanya kazi kwa mtu mmoja muhimu sana katika historia ya muziki wa Afrika Mashariki, mtu huyo aliitwa Peter Colmore. Colmore akamuajiri Ondolo kuwa mtunza store ya vyombo vyake vya muziki.
Niongee kidogo kuhusu huyu Peter Colmore. Colmore alizaliwa Uingereza mwaka 1919, mwaka 1938 akahamia Kenya ili afanye kazi kwenye kampuni ya ndege ya Wilson Airways, lakini ilipoanza tu vita ya pili ya dunia mwaka 1939, mali zote za Wilson Airways zikataifishwa na jeshi la Uingereza, Peter nae akalazimika kujiunga na KAR. Baada ya vita Peter akishirikiana na mtu mwingine mashuhuri katika historia ya muziki wa Afrika ya Mashariki, Ally Sykes, wakaanzisha Colmore African Band. Huyu Mzee Sykes ni babu wa mwanamuziki Dully Sykes. Ni wakati huu huu ndipo John Ondolo Chacha akapata kazi ya kutunza stoo ya vyombo vya muziki vya Peter Colmore.

Baadae Peter Colmore akaanza kazi ya ‘uproducer’ wa muziki na kuwa na lebo yake ambayo ilikuja kutoa santuri zaidi ya 250, lebo hiyo iliitwa His Master’s Voice (HMV) Blue Label.
Colmore pia akanzisha kampuni ya promosheni ya bidhaa iliyoweza kuwagundua wanamuziki wengi akiwemo John Mwenda Bosco na Edward Masengo.
Pamoja na kuwa Ondolo alifanya kazi kwa Colmore, hakuna kumbukumbu kuwa aliwahi kutoa nyimbo zake katika lebo ya Colmore kwani kati ya nyimbo zake za kwanza ni Wazazi Musilie, iliyotoka mwaka 1959 chini ya lebo ya Galotone ya Afrika ya Kusini.
Baada ya hapo John Ondolo alitoa nyimbo kadhaa zikiwemo, Ukiwa Na Bwana We Bibi, Safari Ya Kilimanjaro akiwa na the Jolly Trio Band, Olalekanga akiwa na Jolly Quartet Band nyimbo hizi zilitoka mwaka 1961. Mwaka 1962 alirekodi Yunie Mpenzi We akishirikiana na Jolly Quartet Band na wimbo Kenya Style aliopiga peke yake.
Mwaka huohuo 1962 John Ondolo aliingia jiji la Dar es Salaam kwa mara ya kwanza. Akajiwekea makazi yake eneo la Sombrelo, Ubungo. Sombrello ilikuwa ‘night club’ maarufu wakati huo na bendi nyingi zikipiga hapo, club hiyo ilikuwa pembeni tu mwa jengo la Ubungo Plaza, kwa sasa eneo hilo kumejengwa kanisa kubwa. Ondolo aliweza kupata umaarufu mkubwa kiasi cha kuchaguliwa kuwa Katibu wa wa eneo lile katika muda mfupi sana.
Mwaka unaofuata alirudi tena Kenya ambako pamoja na kuoa mke wake wa kwanza alianza tena kutoa nyimbo. Mwaka 1963 alirekodi wimbo wa Tucheze Selele, mwaka 1964 akatoa Tumshukuru Mungu na Kenya Twist, mwaka 1965 Siri ya kijana, mwaka 1967, Kwela Wangu na mwaka 1968 akishirikiana na Ngambotano Boys Band akatoa wimbo wa Haukutoka Mbinguni.
Mwaka huo huo 1968, akarudi Tanzania akisindikizana na watoto wake watatu. Aliweza kupata kazi katika shamba la Mawingi huko Moshi ambako akafanya kazi mpaka mwaka 1970, ndipo akapata mwaliko wa kurekodi nyimbo kwa ajili ya kuhamasisha utalii na akatoa nyimbo mbili, Kilimanjaro and Mbuga zetu . Nyimbo hizi alirekodi katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Baadae akaajiriwa hapohapo redio kama mtayarishaji wa vipindi vya biashara. Mwaka 1972 akaajiriwa na Umoja wa Vijana wa TANU (TYL) kama Katibu Mwenezi. Na ilikuwa ni hapo kwa kutumia vyombo ambavyo viliachwa na bendi ya wanawake Women Jazz band, akashirikiana na Hamza Kalala kuanzisha Vijana Jazz Band
Tarehe 21 Machi 2008 ilikuwa ni Ijumaa Kuu, John Ondolo alienda kanisani kusali, katikati ya misa alidondoka, akakimbizwa hospitali lakini alipofika hospitali John Ondolo Chacha alikuwa amekwishapoteza uhai.
John Ondolo alizikwa Dar es Salaam, akiwa ameacha watoto kumi na moja.
Mwisho nielezee kwanini magita makavu haya huitwa Magalatoni. Mwaka 1923, huko Afrika ya Kusini ilianzishwa kampuni iliyoitwa Gallotone, pamoja na kuwa ilikuwa label ya muziki pia ilikuwa ikisambaza vifaa vya muziki vilivyokuwa na nembo yake.
Magitaa mengi yaliingia nchini kutoka Afrika ya Kusini kabla ya Uhuru na yalikuwa na nembo ya kampuni hiyo hivyo kuanzisha utamaduni wa kuyaita magitaa yasiyo na umeme Magalatoni.
