SALIM WILLIS MWANAMUZIKI ALIYETOKEA BENDI YA SHULE.

Shule nyingi sana za sekondari,  katika miaka ya 70 na kurudi nyuma, zilikuwa na bendi za muziki wa magitaa. Wengi wa wanafunzi hawa hawakuendelea na kupiga muziki ukubwani, lakini wengine hawakuacha talanta hiyo na maisha yao yakaja kutegemea muziki.
Salim Willis ni mmoja kati ya wanamuziki wa bendi za shule aliyefikia kuwa mwanamuziki wa bendi kubwa maarufu Afrika.
Salim alianza kupata hamu ya kuwa mwanamuziki baada ya kuwa mpenzi mkubwa wa filamu za Elvis Presley. Elvis alikuwa mwanamuziki  Mmarekani mahiri wa muziki wa rock’n’roll aliyetawala anga za muziki wa dunia kwa muda mrefu na hatimae kupewa heshima ya kuitwa Mfalme wa muziki wa Rock ‘n’ Roll. Elvis pia aliigiza filamu nyingi na vijana wengi waliopenda muziki wa Elvis hawakutaka kukosa kuangalia filamu za Elvis, kwani katika filamu hizo Elvis alikuwa pia na vipande vya kuimba, kupiga gitaa  na kucheza.
Salim alianza kuhudhuria mazoezi ya bendi ya vijana wa Kigoa  iliyoundwa na wanafunzi aliokuwa akisoma nao katika shule ya iliyoitwa  St Xavier iliyokuwa Dar es Salaam, siku hizi shule hiyo  inaitwa shule ya sekondari ya Kibasila. Mwanzo alianza kujishirikisha kwa kupiga marakasi. Kwa kuwa hakuwa na ujuzi wa mapigo ya muziki mara nyingi kulitokea ugomvi wenzake wakimtaka aache kupiga kwani alikuwa anaenda tofauti na mkong’osio wa muziki wao, lakini aliendelea kung’ang’ania kupiga marakazi hatimae akawa mahiri kiasi cha kutakiwa kutokosa wakati wa maonyesho ya bendi hiyo.
Salim alihamia shule iliyoitwa Salvatorian  Primary School ambayo baadae ilikuja kuitwa St Joseph ambako huko akakutana wapenzi wenzake wa muziki  na pamoja  wakaanzisha kundi waliloliita the Dynamites, Salim alikuwa mpiga drums wa bendi hii.
 Kundi  la Dynamites lilikuwa na wanamuziki   wafuatao; Abdallah Boja, Bashir Farahani, Mohamed Manyika, Salha, na  yeye Salim Willis. Kwa kadri ya mfumo uliokuwa wakati ule kulikuwa na vikundi vingi vilivyojitambulisha kama ni bendi lakini havikuwa na vyombo.  Vikundi hivi vilifanya mazoezi kwa kutumia magitaa baridi, kisha kila mwisho wa wiki vilizunguka kutafuta zinapopiga bendi kubwa na  huko kuomba nafasi ya kutumia vyombo vya umeme wakati bendi hizi zinapokuwa katika mapumziko kwenye maonyesho yao. Bendi zilikuwa zina kawaida ya kuwa na mapumziko ya nusu saa hivi katikati ya maonesho yao, na hapo ndipo bendi ndogo zilipopewa nafasi ya kuptumia vyombo, utamaduni ulioitwa ‘kuomba kijiko’.  Hivyo Salim na kundi lake la Dynamites nao walikuwa wakizunguka bendi mbalimbali kuomba kijiko.

Salim James Willis


Salim alipohamia St Joseph ndipo wakati huohuo alipoanza kufuatilia bendi ya Sparks ambayo ilikuwa ikipiga ukumbi jirani wa Gateways. Katika maonyesho ya Sparks, Salim akawa anakimbilia chombo chake cha maracas ambacho mara nyingi kilikuwa ahakina mtu akikipiga. Uzoefu wake wa awali wa maracas, uliwafanya wanamuziki wa Sparks wamtambue mapema kuwa anaweza. Wanamuziki wa Sparks wakawa wanaweka kiti cha chuma akawa anapiga huku amesimama juu ya kiti ili aonekana.  Salim akaanza kuwa na hamu ya kujifunza gitaa hasa kwa ajili ya kuupenda sana wimbo maarufu wa Besame mucho. Akahangaika kujifunza mpaka akafikia uwezo wa kupiga wimbo huo kwa kidole kimoja, hii ilikuwa hatua kubwa katika kuonyesha nia ya kutaka kupiga gitaa. Mmoja wa wanamuziki wa Sparks akampa kitabu cha kujifunzia chords za gitaa, pia akamuazima gitaa awe nalo nyumbani, iwe rahisi kujifunza. Hiyo kwake ilikuwa bahati kubwa sana, wakati huo huo akawa anajiendeleza katika drums chini ya mwalimu wake George Muhuto, ambaye alikuwa akimuelekeza mapigo mbalimbali ya drums, na kumpa homework kuwa lazima kufikia kesho yake awe ameyakariri. Akajifunza mapema mapigo ya  Bosa Nova, Chacha, Tango na kadhalika. Na kwa juhudi zake mwenyewe za kuanza kufuatisha mapigo ya santuri za vikundi mbalimbali kama The Famous Flames ya James Brown akawa mpiga drums mahiri.  

Salim Willis akiwa Afro 70


Kwa kuwa ilikuwa lazima awe amerudi nyumbani kwao kabla ya saa nne usiku, akawa anapangiwa kupiga nyimbo za mwanzo mwanzo kwenye onyesho, ambayo mengi yalikuwa yakianza saa nane mpaka saa kumi mchana siku za mwisho wa wiki. Wakati wote huo alikuwa akitoroka tu nyumbani kwao kwa kupitia tundu alilolitengeneza kwa kufumua vigae vya nyumba yao ambayo ilikuwa moja ya kota za relwe pale Gerezani. Baba yake alipogundua kuwa mwanae huwa anatoroka, akamtuma mfanya kazi wao mmoja amfuatilie ajue anaishia wapi, mfanya kazi akarudi na jibu kuwa jamaa anaishia kwenye muziki na anapiga chombo chake vizuri sana. Baba yake hakuchukia ila alimwambia aache kupitia kwenye paa la nyumba awe anatumia mlango. Si muda mrefu baada ya hapo bendi ya Sparks ikafa ikazaliwa bendi nyingine nzuri sana iliyoitwa The Comets, na pia  likaanzishwa pia kundi lililojiita The Gypsies, ambalo alikuwemo yeye Salim Willis, Paul Muhuto, Charles Sabuni, Omari Sykes na Abraham Sykes na Mzanda. Kwa vile kundi lilikuwa halina vyombo, wakaamua kuwafuata Afro70 ambao wakati huu walikuwa wakipiga Princes Bar, na wakatumia njia ileile ya kuomba kijiko wakawa wanapiga wakati wanamuziki bendi ya Afro 70 inapumzika. Hatimae Salim Willis akajiunga na Afro 70, bendi kubwa iliyokuja kujulikana duniani. Hadithi ya Salim James Willis haikuishia Afro 70 Band tu, alikuja kujiunga na bendi nyingine kama Biashara Jazz Band iliyokuwa chini ya King Makusa Juma Ubao, bendi hiyo ilikuwa mali ya Board of Internal Trade (BIT), kwa muda akawa Rainbow connection, bendi iliyokuwa bendi iliyopiga katika hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, alihamia Tropicana Muzika ya Moshi.

2 thoughts on “SALIM WILLIS MWANAMUZIKI ALIYETOKEA BENDI YA SHULE.

  1. Ahsante sana kwa historia ya huyu swahib yangu. Mimi nilijuana naye akiwa Afro 70 enzi za New Palace Bar ambayo baadaye ikawa Mbowe

Leave a Reply to Salimwillis77@gmail.com Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top