Katika mfumo wa awali wa muziki wa rumba hasa kuanzia miaka ya 50, bendi zilikuwa na mfumo wa kutumia magitaa matatu, ambayo yalipewa majina ya gitaa la solo, gitaa la ridhim na gitaa la bezi. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku ridhimm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho gitaa la bezi likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la ridhim na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6, lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la ridhim hunyimwa treble (ukali) kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Mwanzoni mwa miaka ya 60 likaanza kutumika gitaa la nne lililojulikana kama ‘second solo’ au Wakongo waliliita ‘mi solo’. Inasemekana kaka yake mpiga solo maarufu wa Kongo wa enzi hizo Dr Nico, Charles Mwamba maarufu kwa jina la Dechaud ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa hilo la nne. Hili lilikuja kuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na gitaa la solo. Nakumbuka marehemu Ally Makunguru mpiga gitaa maarufu alikuwa anasema gitaa la solo na second solo yanatakiwa kubishana kama mke na mume. Katika mpangilio wa bendi nyingine, gitaa la second solo lilikuwa linajibizana na gitaa la ridhim, katika bendi nyingine gitaa hilo lilikuwa likipiga ‘harmony ya gitaa la solo au ya gitaa la rythm. Cuban Marimba Band chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita ‘chord guitar’, ukisikiliza mpangilio wa magitaa katika nyimbo zake unafurahisha sana. Ubunifu huu uliongeza sana uzito wa muziki na hata kuleta ladha mbalimbali za muziki wa dansi. Na uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa kati ya muziki wa bendi moja na bendi nyingine.

kitime music museum
Ally Makunguru
Lakini katika makala ya leo tuzungumzie gitaa la ridhim. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umuhimu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. Na kujijengea sifa kubwa. Kati ya wapiga gitaa la ridhim maarufu alikuweko Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale, huyu alikuwa Mzambia aliyekuja weka masikani yake katika mji wa Tanga. Alipitia bendi kubwa za Tanga ikiwemo Atomic Jazz Band na hatimae Jamhuri Jazz Band. Satchmo alikuwa na staili peke yake ya kupiga ridhim, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga gitaa la ridhim kwa aina yake kabla ya hapo, lakini hakika wapiga ridhim wengi walichukua mtindo wake na kubuni vionjo vya aina yao. Ufundi wake wa kupiga gitaa la ridhim ulitawala katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band wakati huo. Ufundi wake unaonekana sana katika nyimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina, ambapo kama ilivyokuwa utaratibu zamani kulikuweko na wakati gitaa la ridhim liliachiwa lipige peke yake, wapenzi wa muziki walipenda sana mtindo huo.

Kule Tabora Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji wa gitaa la ridhim uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, wenyewe waliita Segere Matata, gitaa la Kasimu Karuwona ambaye wapenzi wake walimuita Kasim Ridhim, kazi yake inasikika vizuri pale gitaa la solo lilipotulia na kuacha nafasi kwa gitaa la ridhim kwenye nyimbo kama Dada Asha, au Dada Lemmy.
Charles Ray Kasembe aliingia katika ulimwengu wa muziki wa bendi kubwa Tanzania baada ya kuletwa Morogoro na bendi ya Cuban Marimba Band, akiwa Morogoro akahamia Morogoro Jazz Band ya Mbaraka mwinshehe. Upigaji wake wa gitaa la ridhim unasikika vyema katika wimbo kama Wajomba wamechacha. Hao ni wapiga ridhim wachache walioacha alama katika kazi zao. Mwishoni mwa miaka ya 60 ulianzishwa mtindo mpya wa ufungaji wa nyuzi za gitaa la ridhim. Wapiga ridhim wakauondoa uzi namba nne katika gitaa hilo na kwenye nafasi yake wakaweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa moja. Wanamuziki hapa Tanzania ufungaji huo wakauita ‘Double String’. Ni katika zama hizo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa ridhim, mpaka kupewa jina la Mombasa Profesere. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga gitaa la ridhim iliyofungwa ‘Double String’ kwa spidi kali sana, vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Wanamuziki wa mtindo wa Benga toka Kenya waliendeleza vizuri sana upigaji wa staili ya Orchestra Kiam, kwani nao upigaji wao ulikuwa wa spidi kali.
Kama nilivyogusia hapo juu, umuhimu wa gitaa la ridhim ulikuwa ukionekana kwa bendi nyingi katika mtindo wa ‘kuachia ridhim’, huo ulikuwa ni mpangilio ambapo gitaa la ridhim liliachwa lipige peke yake wakati magitaa mengine yakiwa kimya, labda kusindikizwa kwa vichocheo flani na gitaa la bezi. Hapo mpiga ridhim aliachiwa kucheza na gitaa alivyotaka na kuonyesha umahiri wake wote. Mtindo huu ulipendwa sana na wapenzi wa muziki. Utaratibu huu umerudi kwa njia ya ajabu sana, bendi nyingi za taarab zimeurudisha mtindo wa ‘kuachia ridhim’ lakini kwa kuwa bendi hizo hazitumii tena gitaa la ridhim , jukumu hili linafanywa na mpiga solo, na mara nyingi vinapigwa vipande vilevile vilivyopigwa na wapiga ridhim wa zamani katika muziki wa dansi!!!. Kitu cha ajabu ni kuwa matokeo ni yaleyale, wapenzi wa muziki hupanda mzuka na kucheza sana wakati wa kipindi hicho.
Kwa sasa bendi nyingi za dansi hazitilii umuhimu tena gitaa la rythm. Kinanda kimechukua nafasi ya gitaa hili. Kuna bendi ambazo bado zina gitaa la ridhim lakini kwa mfumo wa sasa waimbaji ndio wenye umuhimu kuliko vyombo, hivyo unaweza kumuona mpiga ridhim lakini usisikie anapiga nini. Kwaheri gitaa la ridhim

Nimesoma shule moja na mwanamuziki Abbu Njenga pale shuleni alikuwa na kabendi kake na pia alikuwa na gitaa lake la ridhim na alikuwa mfuasi mkubwa wa Vata Mombasa na Kasembe wa Morogoro jazz, japo baadae akawa pia anapiga solo lakini ridhim ndio hasa lilikuwa gitaa kipenzi la Abbu Njenga.
Hakika huyo ni mmoja wa wapiga rythm wetu
Ahsante sana,,Mzee John kitime Kwa historia nzuri hasa kwenye vyombo ya muziki wa dansi hasa magitaa,,Ombi langu na ushauri wangu Mimi binafsi ningeomba ufanye mpango wa kuandika kitabu Cha muziki wa dansi hapa Tanzania.
Naomba ukipata mda tuandalie historia ya band ya Simba wanyika original chini ya uongozi wake Wilson peter kisaka kinyonga na mdogo wake George peter kisaka kinyonga,hasa kwenye upigaji wa magitaa ya solo na bass, ahsante
Nimefurahia kusoma makala hii. Bila shaka siku moja utakusanya makala hizi na kuzitoa katika mtindo wa kitabu
hakika ntajitahidi