Kumbukumbu zangu huwa zinanirudisha Iringa nilipokuwa na umri wa miaka minne hivi. Nadhani ndipo nilipoanza kutambua kuwa wazazi wangu walikuwa wanajitayarisha kwenda dansini, nakumbuka sauti ya mama ikisema
‘Haya laleni sisi tunaenda dansini’.
Mara ya kwanza kuona watu wakicheza dansi ilikuwa nyakati hizohizo. Pale ulipo sasa Uwanja wa Samora , kulikuwa na shule ya pili ya serikali mjini Iringa. Shule iliitwa Iringa Middle School, na baba yangu alikuwa mwalimu mkuu wa shule ile. Nyumba tuliokuwa tukiishi nayo ilikuwa jirani na shule. Uwanja wa mpira wa shule kwa sehemu kubwa ndio sasa Uwanja wa Samora. Jioni moja uwanja ulianza kupambwa na zikafungwa spika kwente nguzo za miti zilizochimbiwa huku na kule. Yalikuwa ni matayarisho ya ujio wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilikuwa muda mfupi baada ya Uhuru. Mwanga ulikuwa ukitoka kwenye karabai kadhaa ambazo nazo zilikuwa zimetundikwa huku na kule, umeme ulikuwa bado haujafika maeneo ya mengi ya mji wa Iringa. Nakumbuka wimbo mmoja tu kati ya nyingi zilizopigwa siku ile, ulikuwa ni wimbo wa Cubana Marimba wakati ikiongozwa na Salum Abdallah. Ulikuwa na maneno haya, Tutie jembe mpini, Twendeni tukalime. Hapo ndipo nikawaona watu wakicheza dansi kwa mara ya kwanza maishani. Kwa kweli toka nikiwa mtoto, dansi kwangu ni neno la furaha  kwenye maisha yangu. Nikiwa mdogo  wazazi wangu walikuwa wakituonyesha namna ya kucheza aina mbalimbali za dansi, zikiwemo tap dancing, aina ya dansi ambayo viatu lazima uvigonge sakafuni wakati wa kucheza kufuatia mapigo ya muziki, wazazi walitufundisha kucheza  twist, chacha, waltz na aina nyingine za dansi ambazo sijapata hata  kujua majina yake.
Nyakati hizo na miaka mingi baadae, mtu akiaga anakwenda dansini, jambo la muhimu atakalolifanya huko ni kucheza nyimbo nyingi kadri atavyoweza. Kesho yake mazungumzo kuhusu dansini ni kuulizana nyimbo ngapi zilichezesha. Mpenzi wa muziki kurudi nyumbani akiwa kachoka kwa kucheza ilikuwa ndio dalili ya kufurahia kwa usiku ule.
Miaka mingi baadae hatimae nikaja kuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi.  Hii aina ya muziki  ulioitwa muziki wa dansi, ulianza kuitwa hivi wakati wa enzi za Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), nia ilikuwa kuutofautisha na aina nyingine za muziki kama vile taarab , ambayo miaka hiyo ulikuwa muziki ambao ambao wapenzi wake walikuwa hasa wanakaa na kusikiliza ujumbe, pia ilikuwa kutofautisha na   kwaya, muziki wa asili na aina nyingine za muziki. Muziki wa dansi ulitungwa na kupigwa kwa vifaa vya kisasa na nia ya watunzi ilikuwa kuhakikisha wasikilizaji wanacheza.  Katika miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, bendi zilikuwa zikitangaza aina muziki itakaoupiga, kwa mfano kiongozi wa bendi aliweza kutoa maelezo yafuatayo kabla ya kupiga muziki. ‘ Muziki ufuatao unaitwa Dada Adija, umepigwa katika mtindo wa Cha Cha’. Basi muziki ulipoanza wapenzi wa muziki waliingia uwanjani na kucheza Cha Cha tu. Na hivyo hivyo kama wimbo ni Twist, Bolelo, Charanga na kadhalika. 
Tungo za zamani zilikamilishwa kwa muungano wa mawazo kutoka kwa wanamuziki mbalimbali katika bendi. Mtunzi wa awali aliweza kuleta  mashahiri, mara nyingine yakiambatana na melodia na kuwaimbia wenzie ambao walianza kutunga vipande vyao kupitia  vyombo mbalimbali wanavyovipiga. Baadae uliingia utamaduni wa tungo kuanza kwa rumba la taratibu, na ilipofika katikati mwendo ulibadilika na kuingia katika kile tulichokuwa tukikiita ‘chemka’.

Mwalimu Nyerere akilisakata rumba na Bibi Titi


 Chemka mara nyingi ilianza kwa kuimba na kisha kuingia kipande cha gitaa la solo. Hapa ndipo wapiga solo walikuwa wakipimwa kwa umahiri wao wa kutunga na kupiga vipande vya solo ambavyo vingeweza kuwateka akili wasikilizaji na kuwafanya wacheze dansi.
Katika bendi nilizopitia kama vile TANCUT Almasi na Vijana Jazz Band, baada ya bendi kukamilisha wimbo, ulianza kupigwa katika maonyesho mbalimbali, lakini jambo la muhimu ambalo wanamuziki wote tulikuwa tunaliangalia lilikuwa Je, watu wanaucheza wimbo mpya? Ikionekana wimbo  umekosa hamasa ya kuwasimamisha  wachezaji, wimbo huo ulirudishwa mazoezini na kubadilisha vitu tulivyohisi vinafanya watu wasipende kucheza wimbo ule. Na mara nyingine wimbo huo ulitupwa moja kwa moja na kusahauliwa, mamia ya nyimbo  katika bendi mbalimbali ziliishia kupigwa kwenye kumbi mara moja tu na hazikurudiwa tena, kwa kuwa tu watu hawakuchangankia kuzicheza.
Siku hizi mambo yako tofauti kabisa, unaweza kuingia kwenye onyesho la muziki wa Taarab, muziki ambao zamani ulikuwa ukisifika kwa kuwa muziki wa kusikiliza tu, ukakuta wapenzi wakitiririka jasho kwa kucheza nyimbo mbalimbali za Taarab. Na ukaingia katika onyesho la ‘muziki wa dansi’, ukakuta waimbaji wakitoka mishipa ya shingo lakini hakuna anaeshughulika kucheza dansi hilo. Kama ingekuwa  zamani, hiyo ni dalili ya moja kwa moja kuwa muziki huo hauwafurahishi wapenzi. Lakini hizi ni zama nyingine.
Katika zama hizi, bendi huwa na wacheza show wake au hata waimbaji nao wakatengeneza show, kisha wakawa wanapiga muziki na kucheza wao wenyewe. Kwa vipimo vya muziki wa zamani hali hii unaweza kulinganisha na kujitekenya halafu kucheka mwenyewe.

Rumba la taratibu
Kwenye muziki


Teknolojia imeleta aina nyingine ya kuonyesha upenzi na unazi wa muziki. Wapenzi wa muziki siku hizi huonyesha upenzi wao wa muziki kwa kuchukua simu na kurekodi  bendi ikiimba na kucheza, vipande hivi vya video husambazwa kwenye makundi ya Whatsapp, vikiambatana na sifa kuhusu ubora wa bendi hizi.
Pamoja na yote haya, bado  hutokea wapenzi wakachangamkia muziki wa bendi fulani kwa kucheza sana, lakini ukiangalia kila mtu anacheza akili inavyomtuma, hakuna tena mpangilio wa kucheza staili maalumu ya muziki. Ile staili ya wapenzi kukumbatiana kwa hisia wakati wa kucheza rumba imepotea. Wala si ajabu kumkuta mtu anacheza na mpenzi wake, kila mtu na staili yake wakati huohuo kila mmoja anatuma meseji kwenye simu.
Ile sentensi ya kuaga kuwa ninakwenda dansini, kwa sasa imekufa kabisa, utasikia, ‘Naenda kwenye muziki’ au hata ‘Naenda club’. Kwani hakika nia ya kwenda kwenye muziki kucheza haipo tena.

2 thoughts on “DANSI LIMEBADILIKA SANA

  1. Naomba tu nyimbo za zamani zitunzwe katika kumbukumbu kubwa . Upigaji wake, uchezaji wake, hata utunzi wake na mpangilio wa maneno ni hazina kubwa mno. Hsta mavazi ya wanamuziki ni kio tosha. Nyimbo hapa ni muziki wote duniani uhifadhiwe

  2. Umeanza Makala yako kwa maelezo kwamba zamani ilikuwa ni kawaida kwa sisi watoto wa wakati ule kupata elimu elekezi ya muziki kutoka wakubwa zetu walio Wanamuziki au wapenzi wa muziki. Wapenzi wengi wa muziki wa dansi waliujua muziki huo na mitindo yake mbalimbali. Nadiriki kusema wapenzi wa siku zile tulijua ukienda Dansini utakutana na mazingira yepi. Siku hizi wapenzi the wa muziki wa dansi hawana abc za muziki huo na hivyo kujikuta wanacheza muziki wa taarab/bongo fleva/amapiano nk wakijua huo wote ni muziki wa dansi. Hata hivyo kupotea kwa muziki wa dansi sio hapa kwetu tu bali pia kwenye Congo zote mbili. Nawasifu Wenzetu wa Afrika Magharibi ambao wamelinda msingi wa Muziki wa High Life, na Wale wa Latin America. na America ya Kusini kulinda muziki wa Charanga/Salsa. Miziki hiyo ikipigwa leo hii hata na kizazi kipya cha Vijana wao ladha yake ni ile ile. Congo zote zilijidanganya kwa kujitia zinatoka kwenye Rhumba la Asili la Mkongwe Kabasele na kujiingiza katika Rhumba mkorogo. Kinachowashangaza sasa ni huyu Mama Tess ambaye anafanya matamasha kemkem yenye Mafanikio, Ulaya na Marekani kwa kupiga nyimbo zake za zamani na za wakongwe wengineo. Asante, nafurahia Makala zako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top