WAPIGA MAGITAA YA SOLO WALIWEKA NEMBO ZA BENDI

Katika muziki wa dansi wa Tanzania kati ya mwaka 1960 na mpaka 1990,  bendi zilikuwa na utaratibu wa kutumia magitaa matatu au manne. Kulikuwa na gitaa lililoongoza ambalo lilijulikana kama  gitaa la solo, kisha kukaweko gitaa lililosindikiza lililoitwa gitaa la ridhim na kukaweko na gitaa zito lililojulikana kama gitaa la bezi na mwisho kulikuwa na gitaa lililokuwa kati ya gitaa la solo na gitaa la ridhim na hili liliitwa second solo. Au wengine walitumia jina la Kikongo la Mi solo.
Magitaa yote haya yalitokea kuwa na wapigaji maarufu, walioweza kupiga gitaa hilo na kutoa sauti zilizoburudisha sana  wapenzi wa muziki enzi hizo na hata  nyakati za leo. Lakini ukirudi miaka ya nyuma haswa miaka kati ya 1940 mpaka 1960, kabla ya gitaa la solo kuwa ndilo lililoongoza, vyombo vilivyoitwa Mandolin na  Banjo ndivyo vilivyokuwa vinashika nafasi hiyo ya kuongoza muziki.
Mandolini ilikuwa ni aina ya gitaa dogo  lililokuwa na nyuzi nane, banjo lilikuwa nalo chombo cha nyuzi kilichokuwa na nyuzi tano.
Lakini leo ntaongelea gitaa la solo
Kati ya mwaka 1957 na 1960 ndipo magitaa ya umeme yalipoanza kuwa maarufu kwenye bendi za hapa nchini. Dar es Salaam Jazz Band ilikuwa ni kati bendi za kwanza kutumia gitaa la umeme na hili lilikuwa kwa ajili ya kupiga solo tu, inasemekana mwanamuziki mmoja ambaye hutajwa kuwa ni Msukuma aliyeitwa Haus Dibonde ndie aliyekuwa mpiga gitaa la solo la umeme wa kwanza. Huyu awali alikuwa mwanamuziki wa Dar es Salaam Jazz Band, akaja kuchukuliwa na Western Jazz Band, bahati mbaya alikuja kupata matatizo ya akili na hatimae kulazimika kurudishwa kwao.
 Miaka ya mwanzoni wapiga gitaa la solo la umeme walikuwa adimu sana, kiasi cha kwamba wao pekee ndio waliokuwa na uhakika wa mshahara kila mwisho wa mwezi, wapigaji magitaa wengine wote walikuwa wakilipwa posho ndogo mara wamalizapo onyesho.  Mpaka miaka ya karibuni sana bendi zilipokuwa zikifanya kazi ya ziada kumtafuta mpiga solo, alipopatikana alihakikishiwa pato zuri tu,  lakini ilifikia wengi wakaahidiwa hata uongozi wa bendi. Ndio maana bendi nyingi sana viongozi wake walikuwa pia ndio wapiga gitaa la solo. Kupewa uongozi kwa wapiga gitaa la solo kulihakikisha kuwa bendi haitaibiwa   mpiga solo wake. Lakini bahati mbaya si wapiga solo wote waliokuwa na uwezo wa kuongoza bendi, kuna bendi nyingi zilikufa kutokana na uongozi mbovu wa mpiga solo mahiri.
 Wapiga solo wengi walipata umaarufu mkubwa na hakika wengi hawakupata bahati ya kujulikana. Ila hakika wote walichangia sana kwa namna moja au nyingine  katika kuweka nembo za bendi zao. Ilikuwa rahisi kuitofautisha bendi moja na nyingine kutokana na upigaji tu wa gitaa la solo.

Niwakumbushe hapa baadhi ya wapiga solo waliowahi kupata majina makubwa.  Nianze na Rashid Hanzuruni, huyu alipigia bendi nyingi nchini,  baadhi zikiwa Kimbo Twist Band ya Mwanza, Tabora Jazz Band, Dodoma Jazz Band, Kilwa Jazz Band na Western Jazz Band, umahiri wake nyakati zake ulikuwa ukilinganishwa na mpiga gitaa maarufu wa Kongo aliyeitwa Dr Nico. Hanzuruni  hakika alikuwa hodari  kwani aliweza hata kupiga gitaa lililoitwa Hawaian, hili lilipigwa kwa kutereza chuma juu ya nyuzi za gitaa ambalo halikuwa linabebwa begani kama kawaida bali lililazwa kwenye meza wakati wa kupiga. Kwa bahati mbaya, Hanzuruni nae kama ilivyomtokea  Haus Dibonde nae alikuja kupata matatizo ya akili,  miaka hiyo ya nyuma zilikuweko hadithi kuwa yalikuwa matokeo ya ushirikina uliofanywa na waliomuonea wivu kwa umahiri wake.
Bingwa mwingine wa gitaa la solo alikuwa Michael Enoch Chinkumba, aliyejulikana baadae kama King Enoch na mara nyingine Ticha.  Michael Enoch alitokea Zambia, aliletwa nchini na mwanasiasa mkongwe kutoka Mbeya aliyeitwa John Mwakangale. Mwakangale alikuwa na bendi iliyoitwa Free Mwakangale Jazz, alienda Zambia kununua vyombo vya muziki na huko akakutana na Michael Enoch na wenzie watatu akawashawishi kuhamia Mbeya kupigia bendi yake. Michael Enoch alipigia bendi hiyo na baada ya mikasa mingi, akatua Dar es Salaam Jazz band ambayo ilikuwa inatafuta mpiga solo wa kujaza pengo lililoachwa na Haus Dibonde.
Michael Enoch alitoa mchango mkubwa sana katika upigaji wa solo, alijulikana sana kwa uwezo wa kutumia  vyombo viliweza kuboresha mlio wa gitaa la solo (effect). Kulikuwa na vyombo kama tremolo, echo chamber, repeater na kadhalika ambavyo vilifanya solo la Dar es Salaam  Jazz band kuwa tofauti na bendi nyingine.
 Katika wapigaji wa solo huwezi kuacha kumtaja Mbaraka Mwinshehe, huyu alianza kwa kupiga filimbi, akawa anatoroka shule usiku na kwenda kupiga filimbi Morogoro Jazz Band. Siku moja akapatikana kuwa kati ya wanafunzi waliokuwa wakitoroka bwenini usiku kwenda kwenye muziki. Yeye na wenzie wakaamuriwa wapewe adhabu ya viboko, Mbaraka akaamua kuacha shule kuliko kupigwa viboko. Baada ya hapo akaishia kujiunga na Morogoro Jazz band, ambapo baada ya muda mfupi alionyesha kipaji kikubwa cha kupiga kigaa la rhythm kiasi cha wazee wa bendi kuamua kumpa mshahara wa shilingi  125 kwa mwezi, Jambo hili lilimuudhi sana mpiga solo aliyekuweko, kwani aliona ni yeye pekee mwenye haki ya kulipwa mshahara.  Siku chache baadae mpiga solo huyo aligoma kusafiri na bendi kutokana na jambo hilo, mbaya zaidi safari hiyo ilikuwa ni mualiko wa bendi nyingine ya Dar es Salaam kutaka wafanye onyesho la kupimana uwezo.  Mbaraka akalazimika kupiga solo na akaonekana ni mahiri pia wa gitaa la solo, kwanza akapandishwa mshahara na kuanza kulipwa shilingi 250, na ndio akawa mpiga solo rasmi wa Morogoro Jazz Band, mpaka alipoihama bendi.  Aliyoyafanya kwa kutumia gitaa hilo yako wazi kwa kila mpenzi wa muziki wa dansi wa zamani.
Katika miaka ya sitini, bendi zilikuwa umeenea katika karibu kila mji nchini Tanzania, na kila bendi ilikuwa na mpiga gitaa la solo, hivyo walikuweko mamia ya wapiga solo. Si rahisi kuwataja wote lakini katika makala hii kwa vile bendi nyingine zilikuja kuwa maarufu na nyingine hazikuwa maarufu, na hakika nyingine hazikuishi muda mrefu.
Namkumbuka mwanamuziki Abel Balthazar, pamoja na kupiga gitaa mwanamuziki huyu pia alikuwa na uwezo mzuri wa kupiga pia  saxophone, zama hizo chombo hicho lilipewa jina la ‘mdomo wa bata’. 
Historia ya Abel Balthazar ni ndefu sana, kwani  licha ya upigaji wa gitaa la solo pia alikuwa  na uwezo mkubwa wa mipango iliyowezesha kuanzishwa kwa bendi kadhaa  zilizokuja kuwa kubwa na maarufu. Baadhi ya bendi ambazo alizopitia Balthazar  ni Highland Stars Band, bendi iliyokuwa na makao yake Iringa mjini. Balthazar alifanya kazi katika bendi hii lakini hakuwahi kurekodi na Highland Stars, kisha Balthazar alikwenda Kilosa Jazz Band na kuwa mpigaji aliyetegemewa sana. Akiwa Kilosa Jazz Band aliwahi kushawishiwa kujiunga na Dodoma Jazz Band. Aliiacha Kilosa Jazz na kuhamia Dodoma Jazz Band, ambako alikaribishwa vizuri na mazoezi na bendi mpya yakaanza, na kwa vile bendi ilikuwa na sare za suti, na Balthazar nae akanunuliwa suti yake. Katika kipindi hichohicho, wazee watatu walifika kwenye uongozi wa Dodoma Jazz Band,  walikuwa wametumwa toka Kilosa Jazz Band, walimkabidhi kiongozi wa Dodoma Jazz Band barua iliyokuwa ikimtaka Balthazar arudi Kilosa Jazz haraka , kinyume cha hapo madhara makubwa yangetokea. Kwa zama hizo tishio namna hiyo halikuchukuliwa kwa wepesi. Bila kutaka kungojea matokeo, Balthazar alirudishwa Kilosa Jazz Band. Lakini hata hivyo baadae  Balthazar alikuja kuiacha Kilosa Jazz Band kwa njia ya kuchekesha sana. Siku moja Balthazar alifikia uamuzi wa kutoroka.
Siku hiyo Kilosa Jazz band ilikuwa ikipiga katika ukumbi wa Community Center. Honi ya treni ikasikika ikiashiria treni kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam ilikuwa inaingia Kilosa.  Balthazar akafanya jambo ambalo lilikuwa kawaida miaka hiyo, katikati ya wimbo akamwachia mpiga rhythm aendelee kupiga peke yake, ilikuwa niaina ya mpangilio wa muziki zama hizo. Kisha akaweka gitaa lake la solo chini na kushuka jukwaani,  watu wakiwa wanaendelea kucheza,  Balthazar  akapitia alipouficha mzigo wake uliokuwa tayari  na kwenda moja kwa moja kupanda treni na kuondoka Kilosa.  Haijulikanai hali ilikuwaje bendi ilipogundua kuwa mpiga solo hatarudi tena jukwaani.
Balthazar alikuja kuibukia NUTA Jazz Band. Akiwa NUTA Jazz Band Balthazar alipiga solo katika nyimbo ambazo bado zinagusa nyoyo za wapenzi wa muziki wa dansi wa Tanzania mpaka leo. Balthazar aliendelea na kupigia katika bendi zilizokuwa bendi bora nchini kama vile  JUWATA, Dar es Salaam International Orchestra, Mlimani Park Orchestra, International Orchestra Safari Sound na hatimae Magereza Jazz Band.

Abel Balthazar

Bendi nyingine iliyowahi kuwa na wapiga solo mahiri sana ni Western Jazz Band. Western Jazz Band  ilijipa jina hilo kutokana na kuwa muanzilishi wa bendi hii alikuwa mzaliwa wa Jimbo la Magharibi. Wakati wa utawala wa Waingereza, nchi yetu iligawanywa katika majimbo, na kati ya hayo majimbo lilikuwepo jimbo lililoitwa Western Province, lililokuwa likibeba mikoa ya Kigoma, Tabora na Shinyanga. Iddi Nhende mwanzilishi wa Western Jazz Band alikuwa mzaliwa wa Nzega.
Katika uhai wake, bendi hii kila mara ilikuwa na wapiga gitaa la solo mashuhuri sana.  Ukianza na Hausi Dibonde  mpiga gitaa la umeme wa kwanza katika bendi za muziki wa dansi, mpigaji ambaye Western Jazz walimnyofoa  kutoka Dar es Salaam Jazz Band, pia walikuja kuwa na Rashid Hanzuruni, Shamba Ramadhani na Wema Abdallah, wapigaji wote hawa mashuhuri  walirekodi  na Western Jazz Band nyimbo zilizotikisa anga za muziki Afrika ya Mashariki.  Dibonde tu ndie hakuwahi kurekodi na Western Jazz band.  Mtindo wa bendi hii uliiitwa Saboso, japo wapenzi wa mtindo huo walifupisha na kuuita Boso.

Katika jiji la Tanga kulikuwa na bendi kadhaa maarufu kama vile New Star Band, Amboni Jazz Band, Jamhuri Jazz Band na Atomic Jazz Band. Bendi hizi na nyingine nyingi zilizokuwa mji huu ziliweza kutoa wapiga solo maarufu sana.
 Jamhuri Jazz Band ambayo ilianza kama kama kundi lililoitwa Young Nyamwezi Band kwenye mwaka 1955, lilikuja kubadilisha jina, miaka michache baada ya nchi yetu kuwa Jamhuri. Mpiga solo wa Jamhuri Jazz Band alikuwa ni Issa Bendera, ambaye alianza kupiga gitaa la solo alipokuwa Morogoro Jazz Band wakishirikiana na Mbaraka Mwinyshehe. Issa alikuwa akishirikiana na Hassan Rajabu ambaye kabla ya kujiunga na Jamhuri Jazz band alikuwa Amboni Jazz Band, bendi iliyopata umaarufu kwa wimbo wake ulioitwa Kidomidomi.

Jambo moja kubwa katika wapiga solo hawa ni kuwa kila niliyemtaja aliweza kubuni aina yake ya upigaji solo kiasi cha kwamba kila bendi ilikuwa na aina yake ya muziki, na waliona fahari katika utofauti huo.
Kiwanda cha nguo cha Tanzania China Friendship Textile , ambacho kilijengwa na Wachina na kupewa jina la Friendship kuonyesha Urafiki katika ya Tanzania na China, kilijulikana kwa wenyeji kama Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, kama ilivyokuwa kwa makapuni na taasisi za serikali nyingi wakati huo, kiwanda hicho kikaanzisha bendi iliyoitwa Urafiki Jazz Band mwaka 1970.  Mpiga gitaa la solo la bendi hii aliitwa Michael Vicent Semgumi alitokea bendi ya African Quelado kama walivyokuwa wenzie kadhaa waliojiunga na bendi hiyo. Upigaji gitaa wa mwanamuziki huyu ulikuwa wa kipekee sana, alipenda kutumia ‘sound effect’ iliyoitwa Repeater, kazi ya kidude hicho ilikuwa ni kurudia sauti kila uzi wa gitaa utakaopigwa.  Kwanza alikuwa mpigaji mahiri na ile repeater ilifanya  upigaji wake uwe wa kipekee kabisa. Ni vigumu kumpata ambaye ameendeleza umahiri wa Michael Vicent. 
Zamani baadhi ya bendi zilikuwa zikitangaza kazi katika magazeti. Biashara Jazz Band chini ya Juma Ubao, King Makusa, ilitangaza nafasi ya mpiga gitaa mmoja na mpiga kinanda mmoja. Nilikwenda kujaribu kupata nafasi ya kazi ya  mpiga gitaa,  vijana kadhaa tulijitokeza,  kabla ya kuanza usaili kuonyesha uwezo wetu, King Makusa alishika gitaa na kulicharaza,  vidole vyake vikidonoa nyuzi kwa spidi kali, moja kwa moja nikaamua kuwa siwezi hata kujitambulisha kama mpiga gitaa.  Wakati huo nilikuwa napigia bendi iliyoitwa The Oshekas, na nilikuwa napiga kinanda baadhi ya nyimbo, sikuwa mzuri sana lakini ndio hivyo kimjini mjini nikabadili gia angani na kuomba kazi ya kupiga kinanda. King Makusa akawasha kinanda na kukipiga  kwa umahiri mkubwa,  nikaomba ruksa kwenda kujisaidia, niliporudi nikawa nimebadili tena kazi na kujiita muimbaji. Nakumbuka siku ileile tulianza mazoezi ya wimbo ulioitwa Betty, tulipomaliza mazoezi sikurudi tena.

Juma Ubao – King Makusa, wa kwanza kushoto


 Juma Ubao  aka King Makusa alikuwa kiongozi wa Biashara Jazz Band, bendi iliyoanzishwa baada ya kuzaliwa kwa Board of Internal Trade (BIT), ambayo chini yake kulikuwa na Regional Trade Corporations (RTC), na  mfumo huo ukaiuwa State Trading Corporation (STC).  Wakati wa STC kulikuwa na bendi ya akina Marijani Rajabu, Raphael Sabuni, Belino, Ally Yahaya iliyoitwa STC Jazz Band, bendi hiyo ilivunjwa na ndipo kukazaliwa Biashara Jazz Band, ambayo ndio ilikuwa na akina Juma Ubao, Belino, Urembo, Huluka, Ally Jamwaka na wengine. Upigaji solo wa Juma Ubao ulikuwa wa aina yake. Yeye mwenyewe alikuwa mrefu mwenye vidole virefu vilivyokuwa na spidi, na alikuwa na staili yake pekee ya kupiga gitaa  ambayo ilitutisha wapigaji wengine wa zama zake……ITAENDELEA

9 thoughts on “WAPIGA MAGITAA YA SOLO WALIWEKA NEMBO ZA BENDI

  1. Pole sana kwa kukutana na King Makusa. Muziki kwa sasa imebadirika, hata mfumo wa mabendi utapotea muda sirefu.

      1. Makala hii inatukumbusha wapiga gitaa mahiri wa Bendi zetu mbalimbali. Ni Makala inayonifurahisha hasa nikiwakumbuka wapiga gitaa la solo hao na huduma bora walizitoa. Makala itapoendelea usimsahau Duncan Njilima.

  2. Umetoa hustoria mzuri sana ya Abel Batazaar sababu niliona mtu mmoja amejaribu kuandika lakini hakutaja Highland stars nikashangaa. Yeye alikuja baada ya Yakubu aliekua akipiga solo pia kwenye nyimbo za awali naikumbuka ile yenye baadhi ya maneno “unamuona yule ndege,
    Yuko juu ya uaridi,
    Macho yake malegevu,
    Sikia anavyoimba,
    Sita sita mpenzi” n.k.

  3. Yaani nimecheka hadi mbavu zinaniuma kuhusu Juma Ubao King Makusa, Makusa nae sasa ndio nini kuonyesha kiwango anachokitaka watahiniwa wake wakifikie

Leave a Reply to Lazaro Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top